MBUNGE wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), amehoji bungeni sababu za serikali kutangaza utalii wa nchi kwenye noti kwa kuweka picha za wanyama akiwemo nyoka.
Lusinde alihoji kwa maelezo kwamba alama ya nyoka kwa imani ya dini nyingine humaamisha shetani hivyo kuishauri serikali kuweka sura za waasisi wa taifa hili.
Mbunge huyo kijana, alisema hayo jana wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
“Kuna haja gani kutangaza utalii kwenye noti? Tuutangaze utalii kupitia vitu vingine na kwenye noti tuweke picha za waasisi wetu.
“Sasa utakuta kwenye noti picha za wanyama mara nyoka, mara simba…kwa imani za dini nyoka ni alama ya shetani…mimi nadhani mambo haya ndiyo yanayosababisha pesa kutopatikana na kuwafanya wananchi wawe na maisha magumu.
“…Kuhusu suala la matangazo, unaweza kukaa kwenye TV na pembeni kukawa na masheikh kisha linapita tangazo linasema Safari Lager urithi wetu, hebu tukae tukatae vitu hivi kwani baadhi yake vinaliangamiza taifa,” alisema Lusinde.
Mbunge huyo pia alitoa kali bungeni baada ya kutaka mkoa wa Dodoma kupunguziwa majukumu huku akisisitiza kwamba hapo ni Makao Makuu ya nchi.
Katika hoja hiyo iliyowafanya wabunge karibu wote kuangua vicheko, alisema haiwezekani mkoa huo ukawa na gereza maalum la kunyonga wahalifu wote nchini na hospitali kuu ya wagonjwa wa akili hivyo kuiomba serikali kuhamisha kimojawapo.
Hata hivyo aliipongeza bajeti mbadala iliyowasilishwa bungeni na kambi ya upinzani akisema sio kila kitu kinachosemwa na wapinzani kinastahili kupingwa.
Pamoja na mambo mengine alionyesha kukerwa na namna mipango mbalimbali ya serikali isivyotekelezwa na kuwa ndoto akitolea mfano mpango wa serikali kuhamia Dodoma.
Katika hilo, Lusinde alimshauri Spika wa Bunge kuonyesha mfano kwa kuwa wa kwanza kuhamia Dodoma na kwamba anaamini baada ya Spika huyo kufanya hivyo viongozi wengine wa serikali wataiga mfano huo.
(habari kutoka Gazeti la Tanzania daima)
Tags:
Hii kali... Alama ya nyoka kwenye noti inahusiana vipi kusababisha wananchi kuwa na maisha magumu? Nafikiri huyu mbunge anahitaji kwenda kumuona doctor upesi sana. LOL....
© 2022 Created by Tulonge.
Powered by