Tulonge

Na Vitus Ngiliule

Ile sauti ya mama iliendelea kuniita kwa nguvu mno na wakati nikiwa bado nahangaika katika lile giza ili niweze kumuona mama, ghafla ulishuka mwanga mkali sana kutoka juu ukamulika ile ile sehemu sauti ya mama ilipokuwa ikitokea na hapo ndipo nilipomuona mama akivutwa mkono na kaka yangu ili asije mahali pale nilipokuwako. Mama aliendelea kulia kwa uchungu sana huku akinitaja kwa jina na nilijaribu kunyanyua mguu wangu ili nimfuate  nikajikuta nashindwa kufanya hivyo kwani miguu yangu yote ilikuwa imeng’ang’ania chini ya ardhi mfano wa mtu aliyenasa kwenye matope mazito hivyo nikawa sina jinsi tena.

Ule mwanga ulitoweka kwa ghafla kisha nikaisikia sauti ya mama ikiishilia kana kwamba kaka alikuwa ameshafanikiwa kumvuta na kumsogeza mbali na ile sehemu niliyokuwako. Lakini wakati nikiwa bado nimetega sikio langu kwa makini sana ili niendelee kuisikia ile sauti kwani kilikuwa ikisikika kwa mbali sana ghafla nilisikia sauti nyingine tofauti na ile ya mama ikiniita kutokea nyuma yangu, hii sauti haikuwa ngeni masikioni mwangu  kwani ilikuwa ni ya Dada Hidaya, lakini nilipojaribu kugeuka tu ghafla nilishtuka kutoka usingizini na nilipoangaza macho vizuri nilimuona yule dada akiwa ameshikilia taulo pamoja na sabuni ya kuogea.

Alipogundua ya kuwa nimeamka kutoka usingizini akasema, “Nimekuita zaidi ya mara tatu lakini ilionekana umelala usingizi kabisa”,aliongea huku akinitupia lile taulo alilokuwa amelishikilia  pamoja na ile sabuni, “ni kweli dada yangu nilikuwa nimepitiwa na usingizi”,nilimjibu huku nikinyanyuka kutoka kitandani.     Alicheka kwa sauti ya juu sana baada ya kumjibu hivyo kisha akaliendea kabati moja kubwa sana lilikuwamo mle chumbani akalifungua na kunionesha nguo nyingi sana zilizokuwamo mle kabatini. Alitoa baadhi ya nguo akazitupia pale kitandani kisha akaniamuru niingie bafuni kuoga na mara tu nitakapomaliza nichague nguo za kuvaa miongoni mwa zile zilizopo kitandani,    

Aliongea huku akifungua ule mlango wa kutokea kisha akaenda zake. Nilivua zile nguo nilizokuwa nazo kisha nikajifunga lile taulo nikachukua na ile sabuni nikalielekea bafu lililokuwamo humo chumbani nikiwa bado naitafakari ile ndoto pasipo kujua ina maana gani. Haikuchukuwa muda nikawa tayari nimekwishatoka bafuni,nilijifuta maji haraka kisha nikajipaka mafuta yangu ya babycare niliyokuja nayo kutokea nyumbani. Pale chumbani pia  kulikuwa na vipodozi vya aina nyingi sana lakini niliogopa kujipaka nisije nikaharibu ngozi yangu.

Nilichagua suruali moja ya jinsi pamoja na t.shirt nikazivaa, hapa sasa nilianza kujiona wa tofauti sana ukilinganisha ni zile nguo nilizokuja nazo kutokea nyumbani kwani niliziona hazina thamani tena kutokana na vile vilaka vilivyokuwemo karibia kila nguo. Ilikuwa inaelekea majira ya saa moja usiku nikiwa nimekaa pale chumbani naangalia TV mara tu baada ya kumaliza kuvaa zile nguo. Ghafla mlango wangu ulifunguliwa kisha akaingia yule dada akiwa amevalia gauni moja refu lililompendeza pamoja na mkoba unaoendana na hiyo rangi ya gauni, “vipi upo tayari sasa, kuna sehemu nahitaji kukupeleka angalau na wewe ukalijue jiji vizuri”,aliongea yule dada huku akitoa simu yake kwenye ule mkoba. Nilimjibu ya kuwa nipo tayari kisha tukatoka naye hadi kule nje akachagua gari moja ya kifahari sana kisha akaniamuru niingiie tayari sasa kwa kuondoka.

Wakati tukiwa bado tupo ndani ya ile gari , alimpigia simu yule kaka ambaye kwa muda huo alikua bado yupo ndani. Haikuchukua mda yule kaka alifika kisha akawasha ile gari akaitoa nje ya geti tukaanza safari ya kulitembelea jiji. Giza lilikuwa limeanza kuingia kwa muda huo hivyo jiji lilionekana liking’aa sana kwa yale mataa ya umeme, binafsi nilikuwa nimepoteza kabisa muelekeo lakini yule dada alikuwa akijaribu kunitajia baadhi ya maeneo kila tunapopita. Nilijiuliza maswali mengi sana kwanini asingenitembeza wakati wa jioni kabla jua halijazama ili niweze kuliona jiji vizuri  lakini yote haya yalikuwa ni maswali yasiyokuwa na majibu kwa akili zangu za kawaida. Tuliendelea kulizunguka jiji hatimaye tukafika ufukweni mwa bahari  kisha ile gari ikasimama, kwa mara ya kwanza ndipo nilipomsikia dada hidaya akimwita yule dereva “ honey” na hapa sasa ndo nikawa nimepata picha ya kuwa walikuwa ni mtu na mmewe. Mara tu baada ya ile gari kusimama waliniamuru nibaki mle ndani ya gari kisha wao wakatelemka na kuanza kutembea kuelekea baharini, nilijaribu kuwatazama kupitia dirishani ili nielewe wanakokwenda na wakati nikiwa bado nawatazama ghafla walishikana mikono na kuanza kutembea kwa kasi sana kuielekea bahari. Wakati nikiwa naendelea kuwatazama kwa makini sana ili nione mwisho wao ghafla nilihisi mdudu ananitambalia  shingoni na nilipogeuka ili kumtoa nikajikuta nimeteleza kutoka kwenye ile siti hadi chini nikajigonga kwenye paji la uso lakini sikuumia sana ila nilipata kauvimbe kidogo, Wakati nikiwa bado nipo chini ndipo nilipofanikiwa kumwona huyo mdudu kumbe alikuwa ni mende hivyo nikajikuta nacheka peke yangu pale.

Nilinyanyuka harakaharaka kisha nikarudi tena pale dirishani ili niendelee kuwatazama lakini sikufanikiwa kuwaona tena zaidi ya yale mawimbi ya bahari yaliyokuwa yakivuma kwa kasi sana, nilijaribu kufungua ile milango ya gari ili nitoke lakini sikufanikiwa na wakati nikiwa bado nahangaika ghafla niliwaona wakirudi wakiwa wameshikana mikono vilevile kama walivyokuwa wakienda. Nilijikausha kisha nikaegemea siti yangu kana kwamba nilikuwa siwafuatilii. Walifika na moja kwa moja wakaingia ndani  kisha yule kaka akawasha gari tukaondoka maeneo yale ya ufukweni, tuliendelea kukata mitaa hatimaye tukafika hoteli moja ya kifahari sana kwa jinsi nilivyoyatazama mazingira yake.

Tuliingia moja kwa moja hadi ndani ya ile hoteli, na mara tu baada ya kuingia mle ndani kuna kitu kilinishangaza  kwani kuanzia wahudumu hadi wateja wa ile hoteli walikuwa ni waarabu na wasomari hivyo mbongo nilikuwa ni mimi tu. Yule dada aliagiza zikaletwa chipsi kuku pale sahani tatu lakini wakati akifungua ule mkoba wake ili kumlipa yule muhudumu nilifanikiwa kupenyeza macho yangu ndani ya ule mkoba wake ndipo nilipoona maburungutu ya noti za shilingi elfu kumikumi zikiwa zimepangana, nilishusha macho yangu chini kana kwamba sijaona chochote kisha nikaanza kula kile chakula huku nikiziwazia zile pesa kwa mfano mimi leo ndo ningezipata ingekuwaje. Tukiwa bado tunaendelea kula ghafla yule kaka alinyanyuka kana kwamba kuna kitu ameshtuka..

Itaendelea jumatatu ijayo..

Views: 868

© 2022   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*