Tulonge

Na Vitus Ngiliule

Mara tu baada ya kusimama aliigonga ile meza kwa nguvu akitumia mkono wake wa kulia, nilibaki nashangaa nisielewe ni nini kilikuwa kikiendelea pale. Yule kaka alimsogelea dada Hidaya kisha akamnong’oneza sikioni mara ghafla naye alisimama na kuchukua ule mkoba wake kwa haraka sana kisha akanishika mkono na kuniamuru ninyanyuke ili tuondoke katika ile hoteli, niliitikia wito wake nikiwa bado nazitamania zile chipsi kwani nilikuwa nimekula kama robo sahani tu hivi.


Tuliondoka tukaenda moja kwa moja hadi ilipopaki ile gari kisha tukaingia, Yule kaka aliiwasha ile gari akaisogeza mbali kidogo usawa wa ile hoteli akaisimamisha kwenye giza kisha akazima taa zote kana kwamba mtu yeyote aliyekuwa mbali na eneo lile asingeweza kuiona gari. Alishusha kioo cha upande wake wakawa wanatazama maeneo ya ile hoteli, ili kujua kinachoendelea nilijivuta kutoka kwenye ile siti niliyokuwa nimekaa nikafanikiwa kupenyeza macho yangu kupitia kwenye lile dirisha walilokuwa wameshusha kioo hapo ndipo nilipoona hoteli ile ikiwa imezungukwa na kundi la askari wakiwatoa watu waliokuwamo kwenye hoteli wakiwa wamefungwa pingu.


Wale polisi walichukua takribani muda wa robo saa hivi kisha wakatokomea pamoja na wale watu,baada ya kuona wale polisi wamekwisha ondoka yule kaka aliiwasha gari akaigeuza tukafuata ile barabara tuliyokuja nayo. Niliendelea kuwa na maswali mengi sana kutokana na hayo matukio yaliyokuwa kitendawili kwangu lakini wakati nikiwa bado nayafikiria hayo ghafla nilishangaa gari inaingia kwenye ile nyumba ya yule dada, aliipeleka moja kwa moja hadi ile sehemu ya kupaki magari tukashuka na kuingia ndani ya nyumba,tulipofika sebuleni tulipandisha ngazi hadi kule juu kisha wao wakaelekea kwenye chumba chao na mimi nikaelekea kwenye chumba change.Nilipofika ndani nilivua vile viatu vyangu kisha nikajitupia kitandani ilikuwa inaelekea mida ya saa tatu usiku. Wakati nikiwa kitandani nilihisi nimelalia kitu mfano wa karatasi ndani ya lile shuka lililotandikwa na nilipofunua nilishangaa kukuta picha ya mama ikiwa imewekewa alama nyekundu ya msalaba, nilishtuka sana nikajikuta mapigo yangu ya moyo yananienda kwa kasi isivyo kawaida. Niliichukua ile picha nikawa naitazama kwa makini sana ndipo nilipoyagundua yale mazingira mama alipopigwa ile picha ni yale niliyoyaona kwenye ile ndoto niliyoota, lakini wakati nikiwa bado naitazama ile picha ghafla mlango ulifunguliwa kisha akaingia yule dada nikabaki nimeduwaa na ile picha nisielewe nini cha kufanya.Yule dada aliponiona aliongea kwa sauti ya juu sana, “Erick umeanza lini hiyo tabia ya kupekua vitu vya watu”..,nilikosa cha kumjibu hivyo nikabaki nimenyamaza kimya naye hakuishia hapo akaendelea kunifokea pale kisha akaichukua ile picha.

Aliniaga kwa ukali akasema ya kuwa wao wanatarajia kuondoka usiku huo na watarudi usiku wa manane sana hivyo mimi nitabaki pale na ile nyumba, alibamiza ule mlango kwa nguvu sana kisha akaenda zake. Nilibaki pale kitandani na hapo sasa wazo la kutoroka mara tu watakapoondoka lilinijia hivyo nikainuka kutoka kwenye kile kitanda kisha nikalielekea dirisha moja mle chumbani lililokuwa usawa ule wa getini ili niwaone wanavyoondoka halafu na mimi nijiandae kwa ajiri ya kutoroka.

Haikuchukua muda baadae niliwaona wakiingia katika gari moja iliyokuwa imepaki pembeni kabisa karibu na lile geti la kutokea, niliendelea kuitazama ile gari hadi ilipotoka nje ya geti na mara tu geti lilipojifunga nilirudi harakaharaka kisha nikapaki baadhi ya nguo kwenye lile begi langu tayari sasa kwa kuondoka.Nilichukua begi langu nikaliweka mgongoni kisha nikatoka moja kwa moja hadi sebuleni na nilipofika nilijaribu kuangaza macho huku na kule nikaona usalama upo kisha nikauelekea ule mlango wa kutokea nje, lakini nilipoukaribia nilishangaa kuukuta ukiwa wazi hivyo nikasita kidogo nikajaribu kuchungulia nje nikaona usalama upo. Nilitoka nje nikauacha pasipo hata kuurudishia kisha nikaambaa ambaa kupitia zile sehemu zisizokuwa na mwanga kulielekea lile geti la kutokea nje,nilipofika nilikuta lile geti limefungwa hivyo nikajaribu kusogea pembeni kidogo kwani kulikuwa kuna nondo mbili zilizoshikizwa kwenye ule ukuta kuelekea juu. Nilizishika zile nondo kisha nikapanda harakaharaka hadi kule juu, nilijaribu kutazama chini tayari sasa kwa kuruka lakini nilichokiona sikuamini macho yangu kwani kulikuwa na maji mengi sana mfano wa bahari yameizunguka ile nyumba, nilijaribu kutazama pembeni lakini hali ilikuwa ni ile ile kwani hata zile nyumba zilizokuwa jirani sikuweza kuziona.

Nilijikuta nimekuwa mzito sana kwani hata lile wazo la kutoroka lilianza kufifia kwenye akili yangu, nilijivuta taratibu kisha nikarudi tena ndani kupitia zilezile nondo nilizopandia nikaongoza moja kwa moja hadi kwenye ule mlango wa kuingilia ndani, niliukuta ukiwa wazi hivyo nikaingia hadi sebuleni nikaitazama ile saa ya ukutani, ilikuwa inaelekea majira ya tano hivi na nusu usiku.

Wakati nikiwa bado nipo pale sebuleni ghafla nilisikia muungurumo wa gari ikiingia hivyo nikajua fika watakuwa ni wenyewe ndo wamefika, niliondoka kwa kasi sana nikapandisha zile ngazi kuelekea juu na nilipofika niliingia moja kwa moja hadi kwenye kile chumba changu kisha nikavua viatu vyangu pamoja na zile nguo nikapanda kitandani na kujifunika shuka. Haikuchukua muda baadae nilisikia ule mlango wa chumbani ukifunguliwa ikabidi nijikaushe kama mtu amelala usingizi kabisa,sikuweza kumtazama huyo mtu ila nilihisi moja kwa moja atakuwa ni yule dada kwani kuna harufu fulani ya marashi aliyokuwa akipenda sana kuitumia.

Kuna kitu alikitupia pale kitandani kisha akaondoka, nilitulia kama muda wa dakika mbili hivi kisha nikajifunua shuka ili nitazame ni kitu gani alichokitupia pale nikakuta ni simu mpya ambayo ilikuwa imeandikwa kwa maandishi ya kiarabu hivyo sikuweza kuitambua ni aina gani ya simu, niliishika ile simu nikaishia kuitazama tu kisha nikairudisha palepale, lakini ghafla mlango ulifunguliwa akaingia yule dada na kunikuta nikiwa bado nimekaa pale kitandani, “Erick hiyo ni zawadi yako niliyokuletea, nimeshakuwekea na kadi yake moja kwa moja”,aliongea huku akinitazama nami nikamshukuru sana kisha akaenda zake, Niliichukua ile simu nikaiwasha na kweli nilikuta tayari kuna kadi yake mle ndani isipokuwa hakukuwa na jina hata moja kwani ilikuwa ni kadi mpya.

Siku ziliendelea kukatika hatimaye nikamaliza mwezi sasa nikiwa bado nipo kwa yule dada, muda wote nilikuwa nikishinda pale nyumbani peke yangu kwani wao walikuwa wakiondoka kila siku alfajiri na kurudi usiku sana.Zile jitihada zangu zote za kutoroka zilikuwa zimeshagonga mwamba kwani kila nilipokuwa nikipanda juu ya ule ukuta wa nje niliishia kuona maji tu na wala si kingine. Nakumbuka mara yangu ya mwisho kutoka ni ile siku waliyonipeleka kwenye ile hoteli tangu hapo sikuwahi kutoka tena, Nilijikuta tayari nimeshakuwa mzoefu wa ile nyumba kwanzia vyakula nilivyokuwa najipikia.

Nakumbuka siku moja ilikuwa ni mida ya saa nne hivi asubuhi wakati natoka chumbani kuelekea sebuleni, kuna chumba kimoja ambacho kilikuwa na mlango mwekundu nilikikuta kikiwa wazi na haikuwa kawaida kwani sikuwahi kukikuta hivyo hata siku moja, nilikisogelea kile chumba lakini nilipokaribia tu ili kuchungulia..

Itaendelea juma tatu ijayo

Views: 644

© 2022   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*