Tulonge

Na Vitus Ngiliule

Ghafla nilimuona mtoto mdogo mwenye umri wa kama miaka sita hivi akiwa amejifunga shuka jeupe lililokuwa liking’aa sana, nilishindwa kuitambua jinsia ya huyu mtoto kwani alikuwa amejifunika shuka hadi kichwani na kuacha maeneo ya usoni tu yakiwa wazi. Nilishtuka sana nikataka kukimbia lakini akanishika mkono na kuniambia nisiogope, alinivuta kwa nguvu ya ajabu sana hadi nikaingia mle ndani ya kile chumba kisha akaniketisha kwenye kiti kimoja kilichokuwa kimetengenezwa kwa kutumia ngozi.

 

Ule mlango ulijifunga kisha nikaona mwanga mkali sana ukitokea kwenye yale macho ya yule mtoto, aliuelekezea ule mwanga maeneo ya ukutani kisha nikaona picha mfano wa sinema na nilipotazama vizuri nilimuona mama akiwa amejitanda nguo nyeusi akiwa na baadhi ya akina mama ambao walikuwa ni majirani zetu kule Dodoma. Kwa jinsi nilivyowatazama walionekana ni kama watu ambao wanaomboleza tukio fulani la kusikitisha. Ile picha ilitoweka kisha nikaiona picha nyingine ikimuonesha kaka akiwa ameshikilia kitu mfano wa karatasi huku amezungukwa na kundi la watu wengi sana.

Ile picha ilitoweka kisha yule mtoto akarudisha macho yake katika hali ya kawaida, akapaza sauti kwa kusema, “unafahamu ya kuwa wewe ni kama kipofu kwa kuwa haufahamu chochote kinachoendelea katika familia yako kuhusiana na wewe. Nimejaribu kukuwekea hiyo sinema angalau upate picha kidogo ya kinachoendelea huko mtaani kuhusiana na kupotea kwako katika mazingira ya kutatanisha”. Aliongea huku akinitazama usoni lakini hakuishia hapo akaendelea kwa kusema, “Mama yako aliwahi kunikuta nikiwa mtaani na mama yangu tukiomba msaada, nakumbuka alitoa noti ya shilingi elfu moja akampatia mama yangu hakuishia hapo kwani alitoa kile kitenge alichokuwa amejitanda shingoni akamvika mama yangu kwani nguo zake zilikuwa zimechakaa sana, kiukweli sisi hatukuwa binadamu wa kawaida ila tulitumwa kama malaika kuja kupima imani za wanadamu hapa duniani na mama yako alionekana ni miongoni mwa watu wenye upendo wa kweli”. Aliendelea kuongea na kusema ya kuwa hiyo ilikuwa ni siku yangu ya mwisho kuwepo katika hii Dunia kwani yule dada pamoja na yule kaka walikuwa wamepanga kuja kunitoa kafara itakapofika mida ya saa tisa mchana

 

Aliendelea kwa kusema ya kuwa ile nyumba niliyokuwamo haikuwa nyumba bali yalikuwa ni makaburi mawili ya yule dada pamoja na yule kaka, alidai ya kuwa walikufa miaka mingi sana iliyopita katika mazingira ya kutatanisha mara tu baada ya kuwasili Tanzania wakikimbia vita kutoka nchi ya Somalia, alimalizia kwa kusema ya kuwa hayo yote aliyoniambia nitayashuhudia baadae kwa macho yangu, aliongea huku akiufungua ule mlango kisha akaniagiza nikamletee ile pini aliyonipa yule dada.

Niliondoka harakaharaka hadi kule chumbani nikaichukua ile pini kwenye lile begi langu la nguo kisha nikamletea na kumkabidhi, mara tu baada ya kumpa aliniamuru ninyooshe kidole gumba cha mkono wangu wa kulia akakishika na kukichoma na ile pini, damu zilitoka nyingi sana kisha akaniamuru nichore alama ya msalaba kwenye paji langu la uso kwa kutumia ile damu, nilifanya kama alivyoniamuru nikachora ile alama ya msalaba na mara tu baada ya kufanya hivyo aliniamuru nirudi tena chumbani nikapaki vile vitu vyangu vyote nilivyokuja navyo zikiwemo nguo zangu lakini vile vyote ambavyo sikuja navyo nisichukue hata kimoja.Nilifanya kama alivyoniamuru nikaenda kupaki vitu vyangu vyote kwenye lile begi langu nikahakikisha hakuna chochote nilichokiacha.

Nilibeba begi langu mgongoni nikatoka moja kwa moja kukielekea kile chumba alichokuwepo yule mtoto lakini jambo la kushangaza nilipofika nilikikuta chumba kikiwa wazi vile vile ila yule mtoto sikumkuta, nilijaribu kuangaza macho huku na kule lakini sikumwona, wakati nikiwa bado nimeshikwa na butwaa nisielewe nini cha kufanya ghafla niliona karatasi nyeupe iliyoandikwa kwa maandishi mekundu ikiwa juu ya kile kiti kilichotengenezwa kwa kutumia ngozi, niliichukua ile karatasi na kuanza kuisoma nayo ilikuwa imeandikwa hivi, “Najua umeshangaa sana kutonikuta ila hilo lisikupe hofu kwani sipaswi kuwepo maeneo haya kwa wakati huu, unachotakiwa kufanya ni kwenda moja kwa moja hadi kwenye kona ya ule mlango wa kutokea nje kisha usimame hapo hadi wenyeji wako watakaporudi, wakishafika unachotakiwa kufanya ni kuwasubiri waingie kisha utatumia nafasi hiyo kutoka nje kwa ajiri ya kuondoka, hadi kwa wakati huu unaposoma huu ujumbe wapo njiani wanakuja na kuhusu ile pini hupaswi kuwa nayo tena kwa ajiri ya usalama wako hivyo nimebaki nayo mimi, kwa heri ya kuonana na Mungu akubariki sana”, nilijikuta jasho likinitiririka sana baada ya kumaliza kuisoma ile barua.

 

Nilichukuwa hatua kama barua ilivyoniamuru nikaenda moja kwa moja hadi kwenye ile kona ya mlango wa kutokea, ilikuwa inaelekea majira ya saa tisa alasiri nilipoitazama ile saa ya ukutani. Haikuchukua muda wakati nikiwa nimesimama kwenye ile kona ya mlango ghafla nilisikia muungurumo wa gari ikiingia ndani ya lile geti hivyo nikafahamu fika ya kuwa ni wenyewe ndo wamewasiri sasa, niliiendelea kujibana katika ile kona ya mlango hadi walipoingia, nilishikwa na hofu sana nikahisi labda wanaweza kuniona lakini cha ajabu wakapitiliza moja kwa moja hadi kule sebuleni. Sikupoteza muda nikatumia nafasi hiyo kutoka moja kwa moja hadi kwenye lile geti la kutokea nikatumia zile zile nondo mbili kupanda juu ya ule ukuta, nilipofika juu sikuyaona tena yale maji yaliyokuwa yameizunguka ile nyumba isipokuwa niliziona baadhi ya nyumba zilizokuwa jirani.

 

Niliambaa ambaa juu ya ule ukuta nikatafuta sehemu iliyo nzuri nikaruka hadi chini, nilitembea hatua kama tatu hivi ndipo nilipojaribu kugeuka ili kuitazama ile nyumba ili kuona kama kuna usalama lakini nilichokiona sikuamini macho yangu, ile nyuma sikuiona tena ila niliyaona makaburi mawili yaliyofunikwa kwa udongo na nilipotazama vizuri niliyaona maandishi kwenye msalaba mmojawapo wa yale makaburi umeandikwa Hidaya Kelvin, nilishindwa kuelewa waliwezaje kumfahamu kwa jina naye hakuwa mtanzania, haya yote yalikuwa ni maswali yasiyokuwa na majibu katika akili zangu za kawaida.

 

Mapigo yangu ya moyo yalinienda mbio sana nikaanza kukimbia kwa kupitia barabara moja ya vumbi, sikuelewa ile barabara ilikuwa inaelekea wapi kwani maeneo hayo yalikuwa ni mageni kabisa machoni pangu. Wakati nikiwa bado naendelea kukimbia nisijue ninapokwenda ghafla nilikutana na kundi moja la vijana wakanisimamisha, “huyu si ndo yule kijana aliyekuwa anatangazwa kwenye vyombo vya habari ya kuwa amepotea”, aliongea kijana mmoja miongoni mwao huku akinishika mkono kisha wakanichukua moja kwa moja hadi kituo kimoja cha polisi kilichokuwa hapo jirani, walinikabidhi katika kile kituo wakaondoka zao nikabaki pale na wale polisi.

Nililala katika hicho kituo kesho yake habari zikawa tayari zimekwisha sambaa kiasi kwamba baadhi ya waandishi wa habari wakawa wamezipata, haikuchukua muda waandishi wa habari wakawa wamewasiri eneo lile, nilipigwa picha nyingi sana zikasambazwa katika magazeti mbalimbali. Nilitolewa katika hicho kituo kisha nikapelekwa kituo kimoja cha television nikahojiwa pale nami nikaeleza kila kitu kuhusiana na yale mazingira ya kutatanisha niliyokuwepo.

 

Habari ziliendelea kusambaa hatimaye ndugu zangu akiwemo kaka na mama zikawafikia, na kwa bahati nzuri mama alikuwa amekuja Dar-es-salaam kwa ajili ya kunitafuta hivyo akawa amefikia kwa kaka. Nilishinda tena katika hicho kituo kesho yake alfajiri mama na kaka wakawa wamewasiri kuja kunichukua, mama yangu hakuamini kuniona nikiwa hai akaishia kunitazama tu huku akitokwa na machozi ya furaha.

 

Tuliondoka moja kwa moja hadi mahali alipokuwa akiishi kaka tukiwa pamoja na baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa na shauku kubwa sana ya kujua chanzo cha kupotea kwangu katika hayo mazingira ya kutatanisha. Tulipowasiri kwa kaka nakumbuka ilikuwa ni mida ya jioni tulikaa pale sebuleni kisha nikawaelezea mkasa mzima kuanzia mwanzo wa ile safari yangu hadi mwisho wake, na hapo sasa ndipo nilipowakumbuka wale wazee wa kule nyumbani kuhusu ile mada yao ya majini watu waliyokuwa wakiizungumzia, kweli nimeamini lisemwalo lipo.

 

MWISHO

 

Views: 802

Replies to This Discussion

Asante kwa simulizi nzuri.. Kila nilipokuwa naisoma.. nilipata picha flan hivi kama "movie" !! Natumaini wataalamu wa kuandika Movie wakiipata hii wanaweza igiza picha nzuri na watu wakaipenda!!!

Big Up Sana!!!

Asante xana kaka Dixon pa1 na wadau wengine kwa kuikubali kazi yangu naamini tupo pa1 nawapenda xana..,kwa xaxa naomba radhi kidogo majukumu ya kimasomo yamenibana ila nikimaliza natumaini ntakuwa na nafasi nzuri ya kuwaleletea simulizi nyingine ili tuzidi kukifurahia hiki kijiji chetu cha tulonge..!

RSS

© 2023   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*