Tulonge

Na Vitus Ngiliule

Nilipotazama mlango huo wa kuingilia nilimuona yule dereva anangia akiwa ameshikilia ile briefcase nyeusi ya yule dada, alikuja moja kwa moja hadi yale maeneo ya sebuleni kisha akapitiliza na kuanza kupandisha ngazi kuelekea vyumba vya juu. Haikuchukua mda yule dada naye aliingia akiwa na uso wa huzuni sana kwa jinsi nilivyomtazama, alikuja moja kwa moja hadi ile sehemu niliyokuwa nimeketi naye akakaa pembeni yangu kisha akasema, “Erick..! naomba uwe makini sana na ule mzigo wangu niliokupa kwani ile ni siri kubwa sana ambayo huwezi kuijua kwa sasa,” niliitikia kwa kutikisa kichwa kuashiria ya kuwa nimemuelewa. Aliinuka kisha akaenda kufungua friji moja kubwa sana akatoa chupa ya juisi akaniletea pale nilipokuwa nimeketi akaiweka kwenye meza moja ndogo, alinikaribisha huku akimimina ile juisi kwenye glasi,lakini nilipoiona ile juisi kupitia kwenye glasi kuna kitu kilinishtua kwani juisi ilikuwa ina rangi nyekundu damu ya mzee. Kwa harakaharaka sikuweza kujua ni matunda gani yaliyotumika katika kuitengeneza hivyo niliendelea kuwa na maswali mengi sana yasiyokuwa na majibu. Nilimuitikia kwa kusema asante kisha nikaanza kunywa ile juisi taratibu, radha yake ilikuwa ni nzuri sana hivyo hata ile hofu ya rangi nyekundu ilitoweka nikajua itakuwa ni juisi ya kawaida tu.


Aliniacha pale wakati nikiendelea kunywa ile juisi kisha akasema atarudi kuja kunionyesha chumba nitakachokuwa nalala, aliongea huku akipandisha ngazi kuelekea kulekule alikoelekea yule dereva. Nilikunywa glasi moja tu nikawa nimetosheka kwani ile juisi ilikuwa ni nzito sana, haikuchukuwa muda yule dada akawa amerudi kisha akaniamuru niambatane naye akanionyeshe hicho chumba nitakachokuwa nalala. Nilinyanyuka kisha nikachukuwa begi langu la nguo na kuanza kumfuata wakati huo ile pini nilikuwa nimeihamishia kwenye zipu ya pembeni ya begi langu. Tulianza kupandisha ngazi kuelekea vyumba vya juu alikoelekea yule dereva na mara baada ya kufika juu nilistaajabu sana jinsi lile jumba lilivyokuwa limejengwa vizuri kwanzia mpangilio wake wa vyumba, kulikuwa na idadi ya vyumba vitano vyenye milango ya rangi tofauti. Yule dada aliniongoza moja kwa moja hadi kwenye chumba kilichokuwa na mlango wa kijani kisha akakifungua na kuniamuru niingie lakini yeye aliishia pale nje akadai ya kuwa kuna shughuli bado anazifanya atarudi baadaye kuja kunipa maelekezo.


Niliingia kisha nikarudishia ule mlango, mle ndani kulikuwa na kitanda kikubwa sana cha sita kwa sita kilichotandikwa vizuri kwa shuka nyeupe, pia kulikuwa na TV,computer na samani nyingi sana zenye kuvutia machoni. Kiukweli katika maisha yangu hivi vitu vilikuwa ni ndoto na wala sikuwahi kufikiria kama kuna watu wanaishi maisha mazuri hivi. Nilitupia begi langu la nguo kitandani kisha nikavua viatu vyangu nikajilaza pale juu kwa kujiegesha, kiukweli niliwaza mengi sana huku nikijiuliza jinsi ile simu ilivyopotea potea kwani sikuwa na mawasiliano tena na mama wala kaka pamoja na ndugu zangu wengine. Wakati nikiwaza hayo ghafla usingizi ulinichukuwa nikalala fofofo pasipo hata kujitambua na wakati nikiwa usingizini ghafla niliisikia sauti ya mama akiniita huku akilia kwa uchungu sana lakini nilipojaribu kutazama huku na kule sikuweza kumuona kwani kulikuwa na giza nene sana.


Itaendelea jumatatu ijayo...

Views: 609

© 2022   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*