Tulonge

Julius Nyerere

Sote tunaweza kuwa maarufu, tunaweza kuwa chochote tunachotaka . Pamoja na hayo, jambo moja ambalo ni dhahiri itakuwa ni vigumu sana kulifikia ni kuwa maarufu na kuheshimika duniani kote kama ilivyokuwa kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye hivi leo tunakumbuka miaka kumi na moja (11) tangu afariki dunia mnamo tarehe kama ya leo mwaka 1999 kule nchini Uingereza katika hospitali ya Mtakatifu Thomas kwa ugonjwa wa saratani ya damu (leukemia).

Serikali ilipotangaza rasmi kwamba Nyerere hatunaye tena, uchungu na simanzi uliikumba nchi nzima na dunia kwa ujumla hususani kwa wale waliokuwa wanamjua Nyerere na kujua alichokuwa akikisimamia na alichokiamini. Bara la Afrika likawa limempoteza kipenzi chake, mtoto wa Afrika ambaye thamani ya mchango wake katika ukombozi wa bara la Afrika haina kipimo. Mpaka anafariki dunia alikuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha amani barani Afrika.Mfano mzuri ni mgogoro wa Burundi aliokuwa akijaribu kuusuluhisha. Mwenyewe aliwahi kutamka kwamba yeye ni mwafrika kwanza na kisha mjamaa.

Mpaka leo hii jina la Nyerere linabakia kuwa kitambulisho chetu kikubwa .Wakati mwingine zaidi hata ya jina la nchi yetu yaani Tanzania.Wapo watu wanaolijua jina la Nyerere na wala wasijue jina la Tanzania au hata Tanganyika. Haishangazi, alikuwa ni mwana wa Afrika kamili. Kadiri siku zinavyopita, taratibu baadhi yetu, hususani vijana wanaoitwa wa kizazi kipya, wanazidi kulisahau jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Viongozi wetu wengi wa sasa( ingawa wakati wa msiba wake waliahidi kumuenzi kwa hali na mali) wanaelekea kusahau kabisa ahadi zao! Wengi wanabakia kumuenzi kwa maneno na sio vitendo.

Lakini je,sote tunafahamu japo kidogo tu historia ya Mwalimu Nyerere? Uwezekano ni kwamba sio wote,hususani vijana wa sasa. Kwa kifupi na kwa msaada wa vyanzo mbalimbali hii hapa historia fupi ya Hayati Baba wa Taifa;

Julius Kambarage Nyerere

Hayati Baba wa Taifa akisisitiza jambo

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa tarehe 13 Aprili mwaka 1922 huko Butiama mkoani Mara, pembezoni mwa ziwa Victoria,kaskazini mwa Tanzania. Baba yake alikuwa ni Chifu katika kabila dogo la Wazanaki.Nyerere alikuwa miongoni wa watoto wanaosemekana kufikia hadi 26. Baba yake, Mzee Burito Nyerere alikuwa na wake wapatao 22.Alianza shule akiwa na umri wa miaka 12 (ilimbidi kutembea kwa zaidi ya kilometa 26 hadi Musoma mjini ili kupata elimu ya msingi). Kipaji cha uelewa shuleni kilimuwezesha kumaliza kozi ya miaka minne ndani ya miaka mitatu tu. Baadaye mnamo mwaka 1937,alijiunga na shule ya sekondari ya serikali ya Tabora kwa masomo ya sekondari. Alibatizwa katika kanisa katoliki akiwa na umri wa miaka 20.

Kipaji chake cha kitaaluma na kiuongozi kilionekana tangu mapema. Kwa msaada wa waliokuwa waalimu wake pale Tabora (ma-father wa kanisa katoliki) baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kusomea ualimu. Fikra za kimapinduzi na kusaidia waafrika wenzake zilianza kuonekana wazi akiwa Makerere.

Nyumba ya Nyerere

Nyumba aliyojengewa Mwalimu Nyerere na serikali baada ya kustaafu.Ipo Butiama.

Baada ya kumaliza Makerere alirejea Tanzania na kwenda kufundisha (St. Mary’s Secondary School) mkoani Tabora. Mwaka 1949 alipata scholarship kwenda Chuo Kikuu cha Edinburgh kusomea shahada ya pili (Masters) katika historia na uchumi wa kisiasa(History and Political Economy). Alipokuwa masomoni Edinburgh, Nyerere ndipo alipoanza rasmi kuunda mawazo yake ya kiukombozi kufuatia kuanza kujifunza kilichoitwa Fabian Thinking . Mawazo yake ya kuunganisha ujamaa na ujima au maisha ya kijamii ya kiafrika ndipo yalipoanza kujijenga au kujiimarisha.Harakati za kujipatia uhuru kwa nchi ya Ghana zilizokuwa zikiongozwa na Dr.Kwame Nkrumah,anakiri Nyerere katika baadhi ya mahojiano aliyowahi kufanya, zilichangia kuamsha fikra za kujikomboa kutoka mikononi mwa wakoloni. Inasemekana Nyerere ndio alikuwa mtanzania wa kwanza kusomea katika chuo kikuu cha Uingereza na mtanzania wa pili kupata degree nje ya Afrika. Alihitimu mwaka 1952.

Nyerere na mama Maria

Mwalimu Nyerere na mkewe Mama Maria Nyerere.

Aliporejea nchini Tanzania (enzi hizo bado ikiitwa Tanganyika), alianza kazi ya kufundisha masomo ya Historia, Kiingereza na Kiswahili katika shule ya St.Francis’ (sasa Pugu Sekondari). Wakati huo huo akawa amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa TAA(Tanganyika African Association) chama kilichokuwa kimeundwa kusimamia maslahi ya waafrika ingawa tayari kikiwa na vuguvugu la kiukombozi na kisiasa. Hapo ndipo serikali ya kikoloni ilipomlazimisha kuchagua kati ya kufundisha(ualimu) au siasa. Mwenyewe anasema alikuwa amepanga kufundisha kwa angalau miaka mitatu kwanza kabla ya kuingia moja kwa moja kwenye siasa. Hilo halikuwezekana. Akachagua kuwa mwanasiasa na hivyo kuanza mkakati mzito wa kuviunganisha vyama mbalimbali vilivyokuwa na malengo sawa.

Nyerere was a simple man!

Mwalimu Nyerere ndani ya Butiama.

Kazi ya kuviunganisha vikundi mbalimbali vya kisiasa vilivyokuwa vimeanza kutapakaa nchi nzima haikuwa rahisi. Lakini alifanikiwa kufanya hivyo mwaka 1954 kwa kuundwa kwa TANU(Tanganyika African National Union) na yeye kuchaguliwa kukiongoza.

Humo ndimo alimopumzika Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.Tizama na tafakari kwa makini maneno yaliyoandikwa hapo nje.

Aliingia katika bunge la wakati huo mwaka 1958 kabla hajawa waziri mkuu mwaka 1960. Tarehe 1 May 1961, Tanganyika ilipewa uhuru wa kujitawala na Nyerere akawa waziri mkuu wa kwanza. Uhuru kamili ulipatikana mwaka tarehe 9 December 1961. Mwaka mmoja baadaye (1962) Nyerere akawa Raisi wa kwanza wa Tanganyika ilipokuwa Jamhuri ya Tanganyika.

Nyerere,mama yake na mkewe

Mwalimu Nyerere(katikati),mama yake mzazi(kushoto) na mkewe Maria(kulia).Picha hii ilipigwa Novemba 10,1985 Butiama baada ya Nyerere kustaafu.

Julius Nyerere alimuoa Maria Gabriel Magige (Mama Maria Nyerere) tarehe 24 Januari 1953 na walijaliwa kupata watoto wanane. Alipostaafu nafasi yake ya uraisi mwaka 1985 alirudi kijijini Butiama ambako alibakia kuwa mkulima wa kawaida mpaka kufariki kwake Oktoba 14, 1999. Endelea kupumzika kwa amani Mwalimu.

Tanzania note

Sura ya Nyerere katika noti ya Shs 100 enzi hizo.

R.I.P MWALIMU JULIUS K.NYERERE.Views: 1261

© 2022   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*