Tulonge

Askofu Dk Shao akosoa desturi ya Wachagga ya kuzikana majumbani

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao, amekosoa utamaduni wa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro, ambao wengi ni Wachaga, wa kuzikana nyumbani (vihamba) na kusema ni utaratibu wa hovyo.

Akifafanua kauli hiyo juzi, Askofu huyo alielezea hofu ya kupotea kwa mashamba ya mibuni mkoani humo, kutokana na utamaduni uliosababisha ongezeko la makaburi kwenye mashamba hayo.

“Naomba Serikali mkoani, iweke utaratibu wa kudumu wa maeneo ya maziko badala ya watu kuzikwa ovyo majumbani… ardhi hii ni ndogo, lakini bado tunaimega kwa kuzika, hapo baadaye hatutakuwa na
mashamba ya mibuni,” alisema.

Askofu huyo aliiomba Serikali kuelimisha wakazi hao, ili wabadili mfumo wa kugeuza makazi na mashamba yao sehemu ya kuzika ndugu zao, ili kutotumia vibaya ardhi ndogo iliyopo.

Alisema hayo wakati wa harambee ya kuchangia Sh milioni 95 za ujenzi wa Kanisa la Usharika wa Nanjara wilayani Rombo na kusisitiza umuhimu wa Serikali kuweka utaratibu wa maeneo ya kudumu ya maziko.

Kwa mujibu wa Askofu Shao, licha ya hatari ya kupunguza mashamba ya kahawa ambayo ndiyo nguzo ya uchumi wa mkoa, lakini pia utaratibu wa sasa wa kuzikana majumbani, utaathiri vizazi vijavyo na kusababisha vikose maeneo ya ujenzi wa makazi.

Alisema kutokana na mkoa kubuni miradi mikubwa ukiwamo wa soko la biashara la kimataifa la Lokolova na mji wa kitalii wilayani Siha, ni matumaini ya Kanisa kuwa pia Serikali itaandaa utaratibu wa kila wilaya, kutenga maeneo ya maziko ya jumuiya.

Dk Shao alisema iwapo mpango wa kila wilaya kutenga maeneo hayo utashindikana, Kanisa litakuwa tayari kununua ardhi kwa ajili ya waumini wake.

Akijibu ombi hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Aggrey Mwanri, alisema amelisikia na atalifikisha kwa Kamati ya Ushauri ya Mkoa ili ufumbuzi upatikane.

Mwanri pia alishukuru Kanisa kwa kutambua mchango wa Serikali kuleta maendeleo ya wananchi. Katika harambee hiyo, Sh milioni 35.5 zilipatikana.

Chanzo: Gazeti la HabariLeo

Views: 443

Add a Comment

You need to be a member of Tulonge to add comments!

Join Tulonge

Comment by Deoscorous Bernard Ndoloi on September 2, 2013 at 12:25

Nilitegemea Askofu huyu kutoa ushauri mzuri zaidi namna serikali inavyoweza kutumia mapori ya Tanzania ili kuinua maisha ya watu wake hasa kwa kilimo, badala ya kuzungumzia vijikaburi kama suala zito na lenye utata. Kwani kieneo cha kaburi kina ukubwa gani mpaka liwe tatizo? Wachaga huwa wanaenda sehemu za tambarare kulima mashamba makubwa ya mahindi, maharage nk. Na hata hivyo Wachaga navyowajua, wamekuwa wabunifu kutafuta vyanzo mbadala vya mapato; hawategemei ndizi tu. Tuwe na fikra pana zaidi hasa tunapowashauri wanaotegemea mawazo yetu.

Comment by Swedi on August 29, 2013 at 12:36

Nilidhani kuna fact kutoka kwenye maandiko ya kibibilia..

© 2022   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*