Tulonge

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami

WAWILI WAENDA INDIA KIMYAKIMYA, DK CHAMI AWA MBOGO, ASEMA WANAOSUBIRI KUONA WENZAO KWENYE MASANDUKU WATASUBIRI SANA
WAKATI tetesi za kupanguliwa Baraza la Mawaziri zikizidi kupamba moto, hali ya afya ya baadhi ya mawaziri imeelezwa kuwa tete hivyo kulazimika kupelekwa India kwa matibabu.Miongoni mwa Mawaziri hao ni wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami ambaye jana aliibuka na kuwataka watu aliowaita wanye uchu wa kuchukua nafasi yake, waache mara moja kutumia afya yake kupiga propaganda chafu za kisiasa.

Hadi sasa, mawaziri ambao taarifa za kuugua kwao zinafahamika ni pamoja na Profesa Mark Mwandosya mwenye dhamana ya Maji, Naibu Waziri Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe na Dk Chami. Wengine ambao taarifa zinaonyesha kuwa walikuwa nje ya nchi kwa matibabu ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe na Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani.

Ingawa haijafahamika maradhi yanayowasumbua hadi sasa, wadadisi wa mambo ya kisiasa wamekuwa wakichukulia hali ya afya ya baadhi yao kama moja ya sababu inayoweza kuwafanya wawekwe kando pale Rais Jakaya Kikwete atakapoamua kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ili kuwapa fursa ya kupumzika na kuendelea na matibabu.
Dk Chami

Dk Chami alisema jana kwamba tangu arejee kutoka India alikokwenda kutibiwa, afya yake imeimarika na hakuna siku aliyoshindwa kutekeleza majukumu yake huku akisema wanaoeneza uvumi huo ni mahasimu wake kisiasa wanaonyemelea nafasi yake.

Alisema mbali ya kufika ofisini kwake kila siku, alishiriki kikamilifu kwenye Mkutano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano uliomalizika hivi karibuni Mjini Dodoma na kujibu hoja mbalimbali zilizoelekezwa kwa wizara yake.
Aliwalinganisha maadui zake kisiasa na fisi mwenye uchu anayemfuatilia mtu kwa nyuma bila kujali umbali wa safari kwa matumaini ya kuneemeka mkono ukidondoka huku akisema Rais Jakaya Kikwete ndiye mwenye mamlaka ya kuteua mawaziri wake kwa vigezo anavyoona vinafaa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo.

“Nashangaa sana, afya yangu ni njema, imeimarika. Tangu nimerejea kutoka India, sijawahi kwenda hospitali wala zahanati yoyote, naingia ofisini kila siku kuanzia asubuhi na kutoka jioni, nimehudhuria Mkutano wa Bunge, Dodoma na leo nina kazi ya kutembelea viwanda, sasa huku ndiko afya yangu kuzidi kudorora?,” alihoji Dk Chami na kuongeza:
“Suala kubwa hapa ni uwaziri, lakini mtu unaposema fulani anaumwa sana au haumwi lazima usimame katika ukweli.
Hizi ni propaganda chafu za kisiasa zinazoenezwa na baadhi ya watu wenye uchu wa kutaka nafasi hii. Rais ana mamlaka yake ya kuteua mtu kwa vigezo anavyoona vinafaa na mamlaka hiyo haitegemei afya ya mtu. Anaweza kuwa mzima au mgonjwa lakini anateua kwa kadri itakavyompendeza yeye.”

Dk Chami aliwataka wananchi wa jimbo lake la Moshi Vijijini kutokuwa na hofu kuhusu afya yake akisema imeimarika na amejipanga kuongoza mapambano ya kuleta maendeleo.

Chami alirejea nchini mwishoni mwa mwaka jana kutoka India alikotibiwa kwa miezi miwili akiwashukuru Watanzania kwa moyo wa upendo walioonyesha kwake kwa baadhi yao kufunga na kufanya mikesha, kumuombea ili apone.

Kinachomsibu
Akizungumzia ugonjwa uliompeleka India, Waziri huyo alisema alikuwa akisumbuliwa na maumivu upande wa kulia wa kifua chake na alipofika India, ilibidi madaktari wamkate kipande cha nyama na kukisindika ili kutambua bakteria husika baada ya awali, kushindwa kuwabaini.

Alisema wakati akiendelea na tiba hiyo, dawa alizokuwa akizitumia zilimletea athari, iliyosababisha mwili kuvimba. Alisema kifua kilipata ahueni mapema na muda mrefu ulitumika kutibu uvimbe aliopata.
Akiwa katika ziara kutembelea kiwanda cha MMI Steel, Dk Chami alitumia fursa hiyo kuelezea pia afya yake akitamba yupo 'fiti' na hana mgogoro wa kiafya kama baadhi ya watu wanavyojaribu kumshinikiza Rais Kikwete afanye mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

“Nipo vizuri sana na uzito umeongezeka kwa kilo 15. Sasa wale ambao wanafikiria kuwaona wengine katika masanduku (majeneza) watasubiri sana” alisema.

Kombani na Chikawe
WaziriKombani alipelekwa nje ya nchi kutibiwa na sasa amerejea nchini. Awali, taarifa zilisema alipaswa kwenda kufanyiwa upasuaji ambao hata hivyo, haukuwekwa wazi.
Waziri huyo hakuonekana katika Mkutano wa Sita wa Bunge uliomalizika wiki iliyopita na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema ndiye aliyekuwa akijibu maswali ya Wizara Katiba na Sheria.

Jana, taarifa zilizopatikana wizarani kwake zilisema Kombani hajaonekana ofisini kwa takribani wiki tatu.
Baadhi ya vigogo wa wizara hiyo ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini, walisema waziri huyo hayupo ofisini kutokana na kuumwa na kwamba alikuwa nje ya nchi wa matibabu kwa takriban wiki tatu.

Msemaji wa wizara hiyo, Omega Ng’ole alisema hajui kama Waziri Kombani alikuwa anaumwa huku akisema waziri kwenda nje au kutokwenda kwa ajili ya matibabu ni suala binafsi hivyo kushauri atafutwe mwenyewe.

Akizungumza kwa simu, kuhusu afya yake Kombani alihoji: “Unataka kufahamu kama mwandishi au ndugu?” baada ya kujibiwa alisema si jambo baya kwa kiongozi kwenda au kupelekwa nje ya nchi kutibiwa.

“Hivi mtu kuumwa ni jambo la kutangaza kweli… nini cha kushangaza kama mtu akiumwa?,” alihoji.

Alisisitiza kwamba, hakuna ubaya kwa kiongozi yoyote kwenda nje ya nchi kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

“Mtu akienda nje kufanyiwa uchunguzi hiyo nayo ni habari? Hilo jambo kwangu ni mambo madogo tu, hiyo siyo habari bwana,” alisema Kombani na kuongeza kuwa hawezi kusema kama ni mgonjwa au la kwa kuwa hilo ni jambo lake binafsi... “Mimi nakwenda nje kila siku, kila wakati katika shughuli zangu za kikazi na hata siku moja sijawahi kuulizwa na mtu.”

Kwa upande wake, Waziri Chikawe naye anadaiwa kwamba hivi karibuni alikwenda India kupata matibabu. Hata hivyo, haikuelezwa kinachomsibu kutokana na usiri mkubwa uliopo serikalini juu ya matibabu ya viongozi hao.

Dk Mwakyembe
Dk Mwakyembe ambaye amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi na kupelekwa India Oktoba 9 mwaka jana, anatarajiwa kwenda tena nchini humo wakati wowote kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya yake.

Mmoja wa watu wa karibu na Dk Mwakyembe alisema juzi kwamba Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, anatarajiwa kurudi katika Hospitali ya Appolo kwa ajili ya kuangalia kama matibabu aliyopata yamemsaidia kwa kiwango gani.

Ingawa Dk Mwakyembe alijitokeza hadharani katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe hivi karibuni, hali ya afya yake haikuwa ya kuridhisha kutokana na ngozi yake kuonekana imeathirika.

Profesa Mwandosya
Profesa Mwandosya ambaye amekuwa akitajwa kama mmoja wa makada wa CCM ambao wangeweza kuwa tishio katika mbio za urais ndani ya chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015, aliwahi kulazwa katika Hospitali ya Appolo kwa zaidi ya miezi mitatu. Sasa hivi, Waziri Mwandosya nchini India ambako anaendelea kupata matibabu.

Ikulu
Kuhusu taarifa za kuwepo kwa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Kurugenzi ya Mawasiliano imesema wajibu wa kubadilisha baraza hilo uko kwa Rais ikiwa ataona kama kuna umuhimu wa kufanya hivyo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema jana jioni alipokuwa akizungumza na Kituo cha Redio cha Clouds FM na kusisitiza: “Rais atakapoamua kufanya hivyo atafanya kwa matakwa yake mwenyewe.”

Habari hii imeandikwa na Joseph Zablon, Keneth Goliama, Fidelis Butahe na Boniface Meena.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Views: 394

Add a Comment

You need to be a member of Tulonge to add comments!

Join Tulonge

Comment by jemadari mimi on February 17, 2012 at 12:06

mimi na wewe tunastahili kutibiwa hapo muhas kwasababu ni watanzania tusiojua umuhimu wa tiba  bora,lkn wale wananaojiita waheshimiwa wenye kujiona ndio wenye haki yakusema chochote juu yetu lazima watibiwe INDIA tena kwa gharama zetu sisi walalahoi wa nchi hii.

Comment by ILYA on February 16, 2012 at 14:09

Unaona sasa,hao  wanakimbilia INDIA kwa kina Amita Bachani,huwezi kuwaona wakikimbilia Muhimbili.Sijui muhimbili ipo kwa ajili ya kina nani?!!!

Comment by Alfan Mlali on February 16, 2012 at 13:11

Sipendi siasa kwa kweli..

© 2020   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*