Tulonge

MABASI maalumu kwa ajili ya kubeba wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalumu, yanatarajiwa kuanza kufanya kazi jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kukabili tatizo la usafiri kwa kundi hilo.

Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) litaagiza mabasi 2,000 kwa ajili ya kutekeleza mpango huo mwakani.

Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group inayoendesha UDA, Robert Kisena alisema katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake, Dar es Salaam.

Alisema magari yatakayoagizwa ambayo ifikapo Juni mwakani yatakuwa yamefikishwa nchini, yanakidhi baadhi ya vigezo vya mabasi yaendayo haraka. Vigezo hivyo ni pamoja na kuwa na milango miwili na upana unaotakiwa.

Hivi karibuni, Wakala wa Usafiri wa Haraka (DART) ulieleza kuwa, awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi yaendayo haraka utaanza kutoa huduma ifikapo Julai 2015 na utayaondoa katika barabara husika daladala 1,600 na zitahamishiwa maeneo mengine.

UDA pia inajikita kutoa huduma katika maeneo yote ya Jiji. Kisena alikuwa akizungumzia mipango ya muda mfupi na mrefu ya shirika katika kukabili adha ya usafiri, sanjari na uzinduzi wa mabasi mapya 40 ya abiria, yanayoanza kazi leo jijini humo.

Alisema, “Tunashirikiana na kampuni ya kutengeneza mabasi hayo iitwayo Eicher na wakala wake hapa nchini ni Africarriers hivyo tumedhamiria kuondoa adha ya usafiri Dar es Salaam na maeneo ya pembezoni mwa Jiji hili, tuna malengo ya muda mrefu ambayo hadi kufikia mwaka 2017, tutaingiza mabasi 5,000, utekelezaji wake umeanza.”

“Leo (jana) tunaingiza mabasi 40 ambayo yataanza kazi kesho (leo), haya hayahusiki na mabasi 2,000 ambayo hadi kufikia Juni mwakani, yatakuwa tayari kazini, kwa kuwa katika kupigania usafiri wanaoumia na kuteseka zaidi wanawake na watoto, tutakuwa na mabasi maalumu kwa ajili ya wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalumu,” alisema Kisena.

Kisena alisema wanawake wataruhusiwa kupakia mabasi ya watu wote yatakayokuwa yakitoa huduma katika maeneo yote jijini.

Lakini, wanaume hawataruhusiwa kupanda mabasi maalumu ya wanawake ili kutoa nafasi kwa akina mama, watoto na watu wenye mahitaji wakiwemo walemavu, kupata usafiri bila usumbufu wanaokumbana nao sasa.

Kisena alisema mabasi hayo yanagharimu takribani Sh bilioni 200 na kutakuwa na vituo saba pembezoni mwa jiji na kituo kimoja kikubwa kuwezesha wasafiri kupata huduma kwa wakati.

Alisema ili kufanikisha hilo, wanatarajia kumaliza kulipa deni lote la Sh bilioni 17 ambalo shirika linalodaiwa kabla ya Juni mwakani.

Ajira zaja Miongoni mwa utekelezaji wa mipango ya muda mfupi aliyoeleza Kisena ni pamoja na kuingiza katika usafirishaji mabasi 30 na jana mabasi 40 huku akieleza kuwa Oktoba mwaka huu, wataingiza mabasi mengine 100 nje ya mradi wa mabasi 2,000.

Alisema kupitia mradi huo, zaidi ya ajira 8,000 zitapatikana kutokana na basi moja kuhudumiwa na watu wanne. Pia alisema pamoja na kwamba mabasi ya Uda hayana mistari ya kuonesha njia, watayaweka alama maalumu ili abiria waweze kutofautisha.

Alisema hawatapandisha nauli ovyo ovyo hata kama mafuta yakipanda. “Tuna mbinu nyingi za kibiashara, hatutegemea kupandisha nauli ovyo ovyo, niwahakikishie wananchi hasa wakazi wa Dar es Salaam kuwa nauli zetu zitadumu kati ya miaka miwili hadi mitano, tuna mbinu nyingi za biashara kuwezesha hilo,” alijigamba Kisena.

Hisa za UDA Kuhusu hisa za UDA, alisema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuuza hisa zake kwao ili kuliwezesha shirika kujiendesha kibiashara na kufikia malengo ya kuanza kupata faida katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Kwa sasa UDA ina umiliki wa wanahisa watatu ambao ni Simon Group yenye hisa milioni 8.9, serikali kuu yenye milioni 3.5 na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inayomiliki hisa milioni 3.6.

“Tunajua serikali haifanyi biashara, tunakusudia kutoa huduma bora kwa wananchi na ndio maana serikali ipo hatua za mwisho kuuza hisa zake kwetu, nimesikia pia kupitia vyombo vya habari kwamba Jiji nao wanauza hisa zao, hawajatuandikia rasmi nia yao hiyo lakini sisi tupo tayari kuzinunua, ila kama kuna

Mtanzania mwenye uwezo wa kwenda sambamba na uwekezaji wetu, azinunue tu,” alibainisha Kisena.

Alisema serikali itabaki kwenye kukusanya kodi na kusimamia sheria kwa mujibu wa Sheria ya Uda ya Mwaka 1974. Alisema mpango wao ni kurejesha umiliki wa Uda kwa wananchi kwa kuiweka kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kuwawezesha kununua hisa.

Chanzo: habarileo.co.tz

Views: 458

Add a Comment

You need to be a member of Tulonge to add comments!

Join Tulonge

Comment by Omary on August 27, 2013 at 7:14

Yaani mie nawapongeza kwa mpango mzima wa kugeza magari au kutatuwa tatizo la usafiri ila mashaka yangu yapo pale waliposema serikali inampango wa kuua hisa zake zote kwao ili ibaki kukusanya kodi tu kwakweli hapo sina imani napo y? serikari ijitowe? sasa si ni yaleyaleya umiliki binafsi why? waondoe magari ya watu wengine? kama ni kuwekeza nao wamewekeza na wanalipia leseni ya biashara zote ni kodi hizo je wapeleke wapi? magari yao.

Naomba wafikiri kwa mara ya pili kuhusu mke na mume kupanda gari tofauti hilo haliwezekani halijatulia pili bei iwe ya serikali sio ya mfanya biashara ili arudishe pesa haraka.

Kila la kheri katika kutatuwa tatizola usafiri Dar.

Comment by Mama Malaika on August 26, 2013 at 13:17
Omary umesema kweli... Wenzetu wanajali sana watu wao sababu wako karibu nao. Waziri na mbunge (UK) wanatumia daladala kwenda kwenye session ukumbi wa bunge ndio sababu daladala zao ni nzuri zina provide service kwa watu wenye matatizo. Hata uwe mbilikimo bado unapanda daladala bila shida
Comment by Mama Malaika on August 26, 2013 at 13:01
Hii itasaidia iwapo muda wote wataoingia humo ndani ni wanawake, watoto na wenye mahitaji maalamu. Ila isije ikawa ni mradi wa fisadi baada ya muda wakaua soko la daladala ili wapate ku-control the market (public transport) maana mafisadi wajanja sana.
Comment by Dixon Kaishozi on August 26, 2013 at 10:13

Kuna kitu hapo umekisema kaka Omari naunga mkono.. Sasa mtu yupo na familia yake wanaenda mjini... baba anapanda gari jingine.. mama na mtoto nao gari jingine.. watakutana mbele kwa mbele ? hapo kuna kizungu mkuti kidogo!!!! Ila mpango ni mzuri!!

Comment by Omary on August 26, 2013 at 8:44

Pia nawapongeza kwakuwa na lengo jema la kukomesha adha ya usafiri kweli hili lilikuwa tatizo pale Serikali iliposhindwa kusimamia uda ila mbona Mwalimu aliweza? yeye alikuwa anatumia nini? kuweza uongozi na alitunza vyanzo vyote vya mali ya uma vikiwemo viwanda mashirika la uma na nk.

Comment by Omary on August 26, 2013 at 8:40

Hayo mabus ya kubeba wanawake na watoto ndio nayasikia leo na hawajafikiri mara 2 maana huwezi kumtenganisha mtu na mkewe na watoto wake, mabus ya kubeba watu wenye mahitaji maalum ndio wenzetu wanayotumia miaka yote unakuta basi mlango mkubwa mlemavu anapita na baiskeri yake pia bus linashuka na kupanda kutokana na sehemu ya kupakia na ndani ya bus nafasi za wazee zipo nafasi za walemavu na baiskeri zao zipo na za abiria wengine pia zipo ila kwetu ndio tunaliona leo hilo haya ndio maendeleo tunayoyataka, ila nina mashoka serikali ikishauza hisa zake zote basi tena uda itakuwa mali ya mtu binafsi so atapandisha bei atakavyo ninavyojuwa uda ni mali ya serikali so wanatakiwa kuhudumia wananchi wake tena kwa bei ya chini kama ni ongezeko la mafuta haliwahusu wananch kinachotakiwa ni serikali kutowa kodi ya mafuta ya uda ili waweze kuhudumia wananchi kwa bei ya chini na kila mtu aweze kusafiri ajivunie kuwa mwananchi anaejaliwa na serikali yake kwa huduma ya usafiri pia wangetowa kodi ya vyakula vyote vibichi namaanisha vile watu wanavyonunuwa na kwenda kupika majumbani yaani wakifanya vitu hivyo viwili tu kwanza watawasaidia sana wananchi then waangalie vyanzo vingine vya kuingiza kodi mapato Natamani haya nilioyaandika yasomwe na mkubwa mmoja wa nchi na ayafanyie kazi ila ndio hivyo najuwa hizi ni kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji mtoni ila siku moja Mungu atawafunguwa macho na masikio na watatekeleza hili.

© 2020   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*