Tulonge

Mapendekezo ya Mh.Mnyika juu ya Mgawanyo Mpya wa Manispaa za Jiji la Dar es Salaam

Mbunge wa jimbo la Ubungo(Chadema) Mh. John Mnyika

Nimepokea mwaliko wa kikao maalumu cha kikao cha fedha na uongozi wa tarehe 3/01/2014 kikao kufanyika tarehe 06/01/2013 saa nane mchana kujadili mapendekezo ya kuongeza maeneo mapya ya utawala katika Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na ajenda zingine.

Nimeonelea tija kuwasilisha mapendekezo yangu kwa maandishi kwa umma na baadae katika kikao tajwa. Kwa hatua hii, ni fursa kwa kila mwananchi kutoa maoni yake juu ya haya;

Kwa ukuaji wa kasi wa Dar es Salaam ambao ndiyo mji mkubwa nchini Tanzania, jiji kitovu cha biashara na viwanda ambalo kadiri ya takwimu linakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni nne na nusu. Jiji hili limeshika nafasi ya tatu katika miji inayokuwa kwa kasi barani Afrika na miongoni mwa miji kumi inayokuwa kwa kasi duniani.

Ifahamike pia, Jiji la Dar es Salaam ndilo linashikilia asilimia themanini na tatu (83%) ya mapato ya serikali kitaifa na takribani asilimia sabini (70%) ya kodi zote zinazokusanywa nchini Tanzania.

Yafuatayo ndiyo mapendekezo yangu ya wasilisho la nyaraka ya mapendekezo yaliyoletwa katika ofisi yangu toka Manispaa ya Kinondoni;

Mosi, Pendekezo la kutumia “Manispaa” badala ya “Wilaya”:
Kadiri ya wasilisho, imetumika pendekezo la “wilaya”. Ningeshauri na kupendekeza kutokana na uhalisia na ukuaji wa kasi kutumika kwa “Manispaa” badala ya wilaya.

Pili, Pendekezo bora la mgawanyo wa Manispaa:
Katika wasilisho lenye uwepo wa mapendekezo saba. Ninaungana na kuafiki utumiaji wa pendekezo la pili lililowasilishwa la kuwa na Manispaa tano (5) ambazo ni;
i. Manispaa ya Ilala
ii. Manispaa ya Temeke
iii. Manispaa ya Kinondoni
iv. Manispaa ya Kigamboni
v. Manispaa ya Ubungo

Sababu muhimu:
1. Ukubwa kijiografia: Kwa kuongeza wilaya mbili mpya yaani Manispaa ya Kigamboni na Manispaa ya Ubungo hii itasaidia wilaya hizi kuweza kuhimili ukubwa wa eneo wa kijiografia ambalo kwa sasa inaelemea wilaya hizi za sasa yaani Manispaa ya Kinondoni na Manispaa ya Temeke.
2. Ukuaji wa kasi wa jiji: Katika ukuaji wa kasi unaoendelea jiji la Dar es Salaam maeneo yaliyopo katika wilaya hasa ya Kinondoni na Temeke ndiyo ambayo yanaongoza pia katika ukuaji huo wa kasi wa kimakazi na shughuli za kiuchumi kama viwanda na uwekezaji. Hivyo kwa kuwa na Manispaa mpya mbili(Manispaa ya Ubungo na Manispaa ya Kigamboni) zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kusimamia vyema mipango miji, kuujenga vyema mji na kusimamia kihuduma.
3. Uwepo wa mipango ya kuimarisha ukuaji wa jiji kupitia miji ya pembezoni “satellite cities”: tayari serikali imeweka dhamira ya kuimarisha ukuaji wa jiji kupitia satellite cities. Hivyo uwepo wa wilaya mbili yaani Kigamboni (Satellite city Kigamboni) na Ubungo (“Luguruni Satellite City” ndani ya Kata ya Kwembe na Kata ya Kibamba) zitamudu kusimamia vyema ujenzi imara wa satellite cities na pia kuwezesha wilaya zitakazoachwa kama wilaya ya Kinondoni kuwa na ahueni ya kuelemewa na kazi hivyo nazo kusimamia vyema mipango ya ujenzi wa satellite cities zilizomo ktk maeneo hayo

Tatu, Ugawaji wa kata ndani ya Manispaa mpya na kusimamia kata zilizopo:
Katika mapendekezo yaliyowasilishwa, kumekuwa na mgawanyo mpya unaonyang’anya kata ambazo tayari zilikwisha kuwapo katika baadhi ya maeneo mathalani ndani ya Manispaa ya Kinondoni. Mfano wa maeneo kama Kisopwa, Mloganzila. Maeneo tajwa yamekuwa yakihamishwa toka Manispaa ya Kinondoni na kupelekwa Mkoa wa Pwani. Hivyo kukizana hata na dhamira ya kujaribu kuchukua baadhi ya kata na maeneo ambayo yapo katika miji inayokaribia jiji la Dar es Salaam katika dhamira ya kupanua jiji.

Pia, kwa nyakati tofauti tumeshuhudia viongozi wa kitaifa wakitaja mara kwa mara katika hotuba zao na matamko yako maeneo yaliyopo ndani ya Manispaa ya Kinondoni kama eneo la Mloganzila kuyataja kuwa katika Mkoa wa Pwani. Jambo hili si sahihi. Jambo hili limekuwa likiacha maswali mengi kwa wananchi. Ifahamike tu, wananchi hawa wanatambulika chini ya mifumo rasmi tuliyojiwekea inayowatambua kama wakazi wa Manispaa ya Kinondoni.

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha ufafanuzi mpana unawekwa na kusimamia uwepo wa maeneo haya yaendelee kuwapo katika wilaya za Dar es Salaam.

Sambamba, kuna hitaji la haraka na muhimu katika mchakato huu kuhakikisha migogoro ya ardhi ndani maeneo ya Kisopwa na Mloganzila yapatiwe ufumbuzi wa kudumu. Pia kuhakikisha maeneo hayo yanabaki katika kata ya Kwembe kwenye Manispaa inayopendekezwa ya Ubungo.

Nne, Kujifunza toka miji na nchi zingine:
Kuna umuhimu mkubwa wa kupanua wigo wa miji na nchi ambazo tunaweza kuchota uzoefu katika zoezi la kugawa wilaya mpya na kupanua jiji la Dar es Salaam. Mifano minne kadiri ya wasilisho pekee haitoshi. Napendekeza na kushauri kuongeza miji iliyopo katika nchi ifuatayo, miji ambayo inashabihiana na sifa za jiji la Dar es Salaam la ukuaji wa kasi, mifumo wa kiutawala, hali za kiuchumi na kimaendeleo ;
i. Lagos-Nigeria
ii. Johannesburg-South Africa
iii. London-Uingereza
iv. New Delhi-India
v. Shangai, China

Katika kusoma na kuchukua uzoefu toka katika miji iliyowasilishwa katika pendekezo na hii mingine, tusiishie kuangalia mifumo ya ugawaji, ukuzwaji na usimamizi bali pia twende hatua ya kuangalia muundo wa utendaji wa miji hii ambayo yatasaidia sana katika kuboresha muundo wa kiutendaji wa jiji la Dar es Salaam.

Tano, Mapendekezo katika Muundo wa Kiutendaji wa Jiji la Dar es Salaam:
Nakubaliana na hitaji la kuwepo kwa Jiji la Dar es Salaam kama chombo kikuu juu ya Manispaa zote tano zinazopendekezwa zitakazokuwapo Dar es Salaam.

Pia, nakubaliana na kuunga mkono hitaji la Meya wa Jiji la Dar es Salaam kuchaguliwa na wananchi. Hii itatoa fursa katika utendaji na uwajibikaji imara ambayo unaweza kupimwa na wananchi.

Hivi ndivyo majiji ambayo yamepiga kasi ya kimaendeleo kama London (Uingereza) yanajiendesha. Pia hata majirani zetu kama Kenya; nao wametambua mfumo huu na kuuchukua katika Katiba yao mpya.

Pendekezo muhimu; kuna haja ya Jiji la Dar es Salaam likawa juu ya manispaa zote tano zinazopendekezwa na hivyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa isiwe na mamlaka na nguvu kulinganisha na Jiji la Dar es Salaam.

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha pia Jiji la Dar es Salaam linapatiwa mamlaka na madaraka ambayo hayaingiliwi na kuzuiwa na wilaya nyingine zozote zilizopo chini yake.

Sita, kuunganisha mapendekezo ya Muundo wa Mkoa wa Dar es Salaam na mchakato wa Katiba Mpya ya Tanganyika:

Kwa kutambua nchi ipo katika mchakato wa kuandika katiba mpya ya Tanzania. Mchakato ambao utatoa fursa ya uandishi wa katiba mpya ya Tanganyika kuna umuhimu mkubwa wa kuanza kuandaa kisheria hoja za kuwapo ndani ya katiba ya Tanganyika zenye kusimamia Muundo wa Jiji la Dar es Salaam. Huu ukawa ni mfumo wa mfano “modal” katika ngazi za jiji zenye kuhitaji kuwapo katika mfumo wa kikatiba. Hii ikiwamo na suala la Meya wa Jiji kubwa kuchaguliwa na wananchi na mengineyo muhimu.

Kuna umuhimu pia wa kuwepo wa hoja ya kikatiba katika upanuzi na ukuaji wa Manispaa na ngazi nyingine za miji ndani ya Katiba. Hivyo, Katiba ya Tanganyika inahitaji kuwa nguzo muhimu.

Hitimisho:
Naomba wananchi wa Jimbo la Ubungo na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla kutoa maoni yenu ili hatimaye tupate mfumo bora wa kiutawala kwa maslahi na ukuaji wa Jiji letu.

Wenu katika utumishi,

John J. Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo

06 Januari, 2013

Views: 334

Add a Comment

You need to be a member of Tulonge to add comments!

Join Tulonge

Comment by Abasi Mikidadi on January 6, 2014 at 8:22

Manispaa ya Ubungo Mhhhh....... kwa nini kusiwe na Manispaa ya Chanika. Ni mtazamo tu kwani ubungo ni karibu sana na Kinondoni labda Manispaa ya Kibamba.

© 2021   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*