Tulonge

Mwokoaji mwenye kipaji cha ajabu asimulia

Mkazi wa Magomeni, Yusuf Aboubakar  aliyejitolea  kufanya kazi ya uokoaji katika jengo lililoporomoka la ghorofa 16 Mtaa wa Indira Gandhi akiwa amepumzika  baada ya zoezi la kuondoa kifusi na uokoji kumalizika, juzi. Picha na Fidelis Felix.

Dar es Salaam. Siku ya nne baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka, Yusuf Aboubakar ambaye ni mwokoaji wa kujitolea aliyeopoa miili yote 36, amesema alikuwa tayari kufa kwa ajili ya taifa lake.

Akizungumza jana, Aboubakar (26) alisema hotuba ya Rais Jakay Kikwete ilimgusa na alipata hamasa ya kusaidia watu waliokuwa wamenaswa ndani ya kifusi.

“Nilifika eneo la tukio saa 3:30 asubuhi baada ya kupata taarifa za maafa hayo katika vyombo vya habari. Nikakimbia mara moja kuja kusaidia,” alisema Aboubakar.
Kijana huyu, ambaye hajawahi kusoma shule ya msingi au sekondari ingawa alipata mafunzo kidogo ya uokoaji.

Alisema alipofika eneo la tukio  aliomba kuendesha kijiko kilichokuwa kunatumika kwa uokoaji, lakini raia na baadhi ya wanajeshi walimcheka, hakujali.

Alisema aliporuhusiwa alianza kazi na ilipofika saa 8:00 mchana alikuwa wa kwanza kuibua mwili wa kwanza ambao ulikuwa wa mwanamke.
“Ukiniuliza… hata cheti cha darasa la saba sina. Lakini ninajua vitu vingi,” alisema Aboubakar.

Uwezo wa kipekee
Shafii Khalifa, ambaye ni mtu mwingine aliyejitolea kuokoa, alikiri Aboukabar kuwa na kipaji cha ziada cha uokoaji tofauti na wengine.
“Alikuwa anaelekeza tu, ukienda hapo kweli unakuta mwili,” alisema Khalifa.
Khalifa alisema waokoaji wengine walimdharau wakidhani labda ni mwendawazimu, lakini baadaye alikuwa msaada mkubwa katika zoezi zima.

“Hajalala tangu Ijumaa, amekuwa hapa hadi leo (jana) tulipomaliza uokoaji,” alisema.
Aboubakar alisema mwili wa mwanamke huyo ambaye ni mama lishe aliyekuwa akifanya shughuli zake mbele ya jengo hilo, ulikuwa umepasuka tumbo na utumbo wote ulikuwa nje.
Aliendelea kusimulia, ilipofika saa 1:00 usiku aliweza kuopoa miili mingine mitatu na usiku wa manane, miili mingine miwili ilipatikana.

Usiku wa kuamkia jana, miili mingine minne iliyoopolewa na Aboubakar kutoka eneo la varanda ya jengo hilo.

Namna ya kugundua maiti
Aboubakar, mkazi wa Magomeni Kagera, amekuwapo eneo hilo tangu Ijumaa saa 3:30 usiku hadi jana saa 4:00 mchana wakati zoezi linamalizika. Alihusika moja kwa moja na kuopoa miili yote 36 iliyokuwa imefukiwa na kifusi.

“Nina uwezo wa kunusa harufu katika kifusi na kujua kama kuna mwili au la. Cha muhimu ni kumwagia maji juu ya kifusi na unaipata harufu,” alielezea kipaji hicho.

Alisema ili kujua iwapo kuna maiti katika mchanga, unamwagia maji juu ya kifusi, kisha unaifuata harufu ya vumbi inapoelekea na utajua iwapo eneo hilo lina mwili au la.
Aboubakar alisema aliwahi pia kusaidia kuopoa miili ajali ya meli ya Mv Skagit, visiwani Zanzibar.

Alisema katika maiti zote 36, wanawake walikuwa watatu, mamalishe wawili na mwanamke mmoja ambaye anaonekana alikuwa mpitanjia.

Aboubakar ambaye licha ya   kutopata elimu yoyote, ana uwezo wa kuzungumza Kiingereza na Kiarabu kwa ufasaha.

Mkandarasi wa Kampuni ya Strabag, ambaye alishiriki uokoaji kwa kiasi kikubwa, Petter Modgran  alikiri na kumsifu Aboubakar kwa jinsi alivyojituma.
“Nimemuuliza iwapo amewahi kusomea uokoaji, lakini anasema hajawahi,” alisema Modgran.

Alipata mafunzo Uganda
Hata hivyo, Aboubakar alisema aliwahi kupata mafunzo  mafupi ya kijeshi Kapiripiri, Uganda   jinsi ya kutambua maiti zilizofukiwa kwenye kifusi,  juu ya mti au  majini.

Kwa nini ameamua kujitolea kuokoa?
Alipoulizwa nini hasa kilichomsukuma kutumia siku nne kwa shughuli za uokoaji, Aboubakar alisema ni kitu anachokipenda katika maisha yake.

“Nipo tayari kufa kwa ajili ya kuokoa watu wa taifa langu,” alisema.
Aboubakar alisema anachofanya katika maisha yake yote ni kusali, kutenda mema na kusaidia watu wenye matatizo.

Chanzo: mwananchi.co.tz

Views: 650

Add a Comment

You need to be a member of Tulonge to add comments!

Join Tulonge

Comment by Christer on April 3, 2013 at 11:33

Rais amewaalika wote waliohusika na uokoaji kwny chakula cha mchana IKULU tarehe 8 mwez huu, list hiyo sijui Aboubakar yumo, maana wasije wakaandikana wadosi waliokua wanasimama tu na waokoaji waKaachwa! Hongera sana Aboubakar, hao waliokua wanakucheka sasa HESHIMA!!!!!!!!!

Comment by Dixon Kaishozi on April 3, 2013 at 11:26

Mungu Akuzidishie kwa kile unacho hitaji.

© 2021   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*