Tulonge

Nauli mpya za Kivuko cha Kigamboni zaanza kutumika rasmi leo.

Pamoja na kuwepo na pingamizi toka kwa Wananchi wa Kigamboni na Mbunge wao Mh. Faustine Ndugulile, serikali imetangaza rasmi kuanza kutumika leo (1/1/2012) kwa nauli mpya za kivuko ambazo zipo juu zaidi ya zile za kwanza kwa madai kuwa gharama za uendeshaji wa kivuko zimepanda.

Bei hizo zilisomeka kama ifuatavyo ukilinganisha kuwa zimepanda kwa asilimia 100 katika kila upande.

Watoto hadi miaka 14 Tsh 50

Watu wazima Tsh 200
Baiskeli Tsh 300
Bajaj Tsh 1,300
Pikipiki Tsh 500
Gari ndogo ya kawaida Tsh 1,500
Pick up (pia huwekwa katika kundi hili station wagon, gari aina ya LAnd cruiser , n.k) Tsh 2,000
Basi Dogo Tsh 3,500
Magari ta tani mbili na trekta tsh 7,500

Mwanafunzi akiwa na sare za shule-Bure


Mambo ya kujiuliza:

-Kwa kuzingatia kipengele hiki "Watoto hadi miaka 14 Tsh 50". Inamaana hata ukiwa na mtoto mchanga itabidi umlipie hiyo Tsh 50?

-Mwanafunzi asiye na sare lakini ana kitambulisho hawezi ruhusiwa kuvuka bure?

-Mapendekezo ya Mbunge wa Kigamboni kwenye barua yake hapo chini yalipigwa chini kimya kimya?OFISI YA MBUNGE WA JIMBO LA KIGAMBONI

Kumb na: KIG/KVK/VOL.1/4 29 Disemba 2011

Mhe. Dkt John P. Magufuli (MB)
Waziri Wizara ya Ujenzi
Dar es Salaam
YAH: KUSUDIO LA ONGEZEKO LA VIWANGO VYA NAULI KATIKA KIVUKO CHA KIVUKONI-KIGAMBONI
 

Wananchi wa Jimbo la Kigamboni wamepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kusudio la kuongeza nauli za abiria, magari na vyombo vingine vinavyotumia huduma ya kivuko kati ya Kigamboni na Kivukoni kuanzia tarehe 1 Januari 2012. 

Kivuko hiki ni kiungo muhimu kwa wananchi wanaoishi upande wa Kigamboni ambao wengi wao ni watu wa kipato duni na hawana ajira za kudumu. Ongezeko la nauli kwa asilimia 100 ni kubwa sana na litawaathiri kiuchumi. Nimepigiwa simu nyingi na kuletewa malalamiko mengi katika siku ya leo kuhusiana na mpango huu wa kuongeza nauli. Wananchi wanataka kujua ni vigezo gani vilivyotumika kufikia nauli hizi mpya; vyombo gani vilivyopendekeza, kupitisha na kuidhinisha nauli hizi na wanataka kujua kwa nini hawakushirikishwa katika mjadala wa nauli mpya. 

Pamoja na ongezeko kubwa la wakazi na magari yanayotumia huduma ya kivuko, cha kushangaza ni kwamba mapato kwa siku yamekuwa ni takribani Tsh 8 milioni kwa siku kwa muda mrefu sasa. 

Ni dhahiri kumekuwa na upotevu mkubwa mikononi kwa watumishi wasio waaminifu wa kivuko. Mapato mengi yanapotea kwa njia zifuatazo:
1. Baadhi ya watumishi wa kivuko kukatisha risiti hususan za magari kwa kutumia vitabu bandia.

2. Baadhi ya watumishi kuziuza tena tiketi zilizotumika badala ya kuzichana.
3. Baadhi ya watumishi na askari wanapitisha magari na abiria baada ya kupokea malipo ya pembeni.

Vilevile mafuta ya vivuko huuzwa kwa wavuvi wadogo wadogo katika maeneo ya Feri.
Mambo haya yote yanafanyika pasipo kificho, binafsi nimeshawahi kushuhudia yote niliyosema hapo juu yakifanyika na kuyatolea ripoti kwa uongozi wa kivuko.
Ninaamini kuwa hatua zifuatazo zikichukuliwa mapato ya kivuko hiki yanaweza kufika zaidi ya Tsh 13 milioni kwa siku:

4. Kudhibiti uuzaji wa tiketi za abiria na magari.
5. Kudhibiti ununuzi, utunzaji na matumizi ya mafuta yanayotumika kwenye vivuko.
6. Kudhibiti idadi ya watu na magari yanayovuka bila kulipia huduma hii.
7. Kupunguza gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vibarua.
Kutokana na unyeti wa suala hili, nashauri zoezi hili lisitishwe ili kutoa fursa ya kujadiliana kuhusu upandishaji wa nauli na maboresho ya huduma hii kwa kushirikiana na wadau na wawakilishi wa wananchi katika Jimbo la Kigamboni.

Natumaini mapendekezo haya yatafanyiwa kazi ili kuepuka kuwabebesha mzigo wa gharama za uendeshaji wakazi wa Kigamboni wanaotumia huduma ya kivuko pale Feri.
Naambatanisha nakala ya barua yangu ya tarehe 19 Januari 2011 yenye kumbukumbu namba KIG/KVK/VOL.1/1 kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TEMESA ambayo ilitoa mapendekezo ya njia ya kuboresha huduma na vile vile kutaka ushirikishwaji wa wadau katika suala la ongezeko la nauli. Barua hii haijajibiwa hadi hivi sasa.

Natanguliza shukrani zangu za dhati.
Wako katika ujenzi wa Taifa

Mhe. Dkt Faustine Ndugulile (MB)
MBUNGE

Nakala:
1. Mhe. Mizengo Pinda (MB)-Waziri Mkuu
2. Mhe. Mecky Sadick-Mkuu wa Mkoa Dar Es Salaam
3. Waheshimiwa Madiwani wote-Jimbo la Kigamboni
4. Wenyeviti wa Serikali za Mitaa-Jimbo la Kigamboni
5. Mkurugenzi Mkuu-TEMESA

Views: 1011

Add a Comment

You need to be a member of Tulonge to add comments!

Join Tulonge

Comment by chaoga on January 2, 2012 at 14:12

ndio mshaambiwa huwezi lipa hiyo nauli PIGA MBIZI UVUKE au kazungukie kule mbagala... ha ha ha ha lakini jamani hamuoni kwamba nauli ilikuwa ndogo sana? mbona vivuko vya kule ifakara na huko kwingineko watu wanalipa nauli zaidi ya hii tangu mwaka 97 nasikia nauli ya kigamboni haijapandishwa tangu miaka 14 iliopita. dismas kama huwezi piga mbizi hamia magomeni

Comment by Bonielly on January 2, 2012 at 11:18

KWENYE SWALA NA VIOMBO KAMA MAGARI BAJAJ MAGUTA HAPO WAZEZIDISHA MNO,

Comment by Mama Malaika on January 1, 2012 at 19:50

Na kwanini hiyo ya watoto sh 50 isiwe hadi kwa wale wenye umri wa miaka 18 maana nao bado wanakuwa shule... Tanzania imeoota meno jamani. Khaaa.......

Comment by Mama Malaika on January 1, 2012 at 19:48

Haya nikiwa na gari 4wheel hiyo sh 2,000 ni kwenda tu au nakurudi? Kwa mtaji huu... basi kiwanja changu cha Kingamboni ntakiuza. 

Comment by ILYA on January 1, 2012 at 17:35

Pale kivukoni kuna uchumi mkubwa sana,kila siku yanakusanywa mashinggi ya kutosha na ndio maana hakuwezi kuwepo plan za kujengwa daraja maana kuna wanene wanavuta michuzi pale.

Comment by ILYA on January 1, 2012 at 17:32

Gari ndogo ya kawaida sh.1500, wale watu wenye tabia tabia ya kwenda kula upepo baridi na mwanana wa bahari maeneo ya huko kigamboni kwenye Mabeach  kwa mtindo huo si mabadiliko hayo ya nauli si yanamalengo ya kuwafilisi,mi naon ahuu ni wizi wa kupitia nyuma ya pazia,huwezi kuweka nauli yote hiyo kiasi hicho wakati sehemu yenye masafa yake sio marefu kihivyo na kunawezekana kutengenezwa daraja ili kuepukana na uzito wa kuendesha kivuko.Tangu kivuko kimeanza kazi ya kuvusha hadi leo ina maana kama hela zingelikuwa zinakusanywa ili kujenga daraja  la kisasa maeneo hayo kungeshindikana kitu gani??

Hamuwezi kuendesha kivuko  lete plan za kujenga daraja, sio hasira kuishia kwa wananchi kwa kuwapandishia nauli wakati uchumi wenyewe ndio kama huo wa kulenga kwa manati.

Temeeni huko Japan au Uchina ( au Vyetinam tehtehteh!! ) msaini mikataba ya kujengewa madaraja maeneo kama kigamboni ili mtuepushe na karaha ya kupandishiwa manauli kihivyo.

Comment by ILYA on January 1, 2012 at 17:17

@ Mambo ya kujiuliza:

-Kwa kuzingatia kipengele hiki "Watoto hadi miaka 14 Tsh 50". Inamaana hata ukiwa na mtoto mchanga itabidi umlipie hiyo Tsh 50?

---------------------

Kuhusu hili itabidi tutoane meno pale kigamboni maana mimi mwenyewe ndio kwetu huko.Meno yatang'oka ikiwa hawatarekebisha hapo.!!!


Comment by Gratious Kimberly on January 1, 2012 at 1:37

Hiii noma sasa...kazi kweli kweli.....sasa kama mtu anakaa kigamboni alafu anafanya kazi tuseme Ilala au mwenge, hiyo nauli tu kwa mwezi si itammaliza, alafu ukute mshahara wenyewe ndo wa kazi zile kama za ulinzi si inakua ni kasheshe hapo. hapo kwenye suala la wanafunzi kwanza wao ndo wataumizwa sio wanafunzi...maanakama kuna vijana huko kigamboni na wana mishemishe town za kila siku...basi dawa ananunua uniform mtu anakua anakatiza hapo kiulaini   akifika town anabadilisha tu!!!

© 2020   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*