Tulonge

Nililala nikiwa naona, nikaamka na upofu

“Wengi wetu tunaishi bila kujiuliza maswali kama; “Itakuwaje iwapo siku nitaamka nikiwa sina uwezo wa kuona tena? Hatujiulizi maswali kama haya kwa sababu tunavichukulia vitu muhimu kuwa vya kawaida tu.”

 

“Hata mimi nilikuwa mmoja kati ya watu hao hadi Januari 2008, nilipopoteza uwezo wa kuona, mama yangu alikuja kuniamsha lakini jibu langu lilikuwa; siwezi kuona, siwezi kuona,” anaanza kusimulia Margareth.

 

Miaka sita iliyopita Margareth Maganga alikwenda kulala akiwa binti mwenye afya njema na furaha tele, lakini asubuhi ya siku iliyofuata aliamka akiwa na ulemavu wa kutooona. Kwa kijana wa umri wa miaka 19 tu, lilikuwa ni tukio la kutisha, kukatisha tamaa na kutia simanzi.

 

Ilikuwa Ijumaa ya Januari 11, 2008 mama yake Margareth alipokwenda kumwamsha binti yake kwani alikuwa amelala hata baada ya muda wake wa kawaida kuamka kuwa umepita.

 

“Mama aliingia chumbani kuniamsha na kuhoji kwa nini nilikuwa nimelala mpaka muda huo, nilimwambia sijaamka kwa kuwa bado ulikuwa usiku, mama aliniambia tayari ilikuwa ni saa mbili asubuhi. Nilifikicha macho kutazama, lakini sikuona kitu...; Nilibaini kuwa nimepoteza uwezo wa kuona,” anasema Margareth.

 

Binti huyu ambaye sasa ana umri wa miaka 25 anasema kuwa mwanzoni alipopoteza uwezo wa kuona alihisi dunia imemwelemea kutokana na ukweli kwamba, alianza kuona matarajio yake ya kuwa mwanasheria yamepotea.

 

“Kilikuwa kipindi cha mateso kwangu na familia yangu, ingawa wao walijaribu kutoonyesha hofu ili kunipa nafuu. Lakini maswali kutoka kwa rafiki na kuishi kwa kutegemea msaada kwa kila ninalotaka kufanya, vilinifanya nikate tamaa,” anasema Margareth.

 

Anaongeza kuwa alikosa raha kila alipokumbuka kuwa hawezi kutimiza ndoto zake, lakini alipiga moyo konde na kukubali hali yake, ingawa haikuwa rahisi kwake ukilinganisha na ndoto alizokuwa nazo.

Safari gizani

Pamoja na kuwa katika kipindi kigumu cha maisha yake, Margareth ameandika kitabu kiitwacho A Journey Through Darkness ambacho anaelezea safari yake tangu alipopoteza uwezo wa kuona.

 

Katika kitabu hicho anasimulia jinsi alivyoanza kupata maumivu makali akiwa nchini Taiwan katika Kongamano la Vijana (World Youth Conference for Adventist Youth),  alipoanza kupata homa kali na maumivu ya misuli.

 

“Sikutaka kuonekana mgonjwa, nilijikaza. Hata hivyo, nilizidiwa na wenzangu walinipeleka hospitali. Majibu yalionyesha kuwa nina upungufu wa damu hivyo niliambiwa kuna aina mbili za matitabu ya haraka;  moja ilikuwa kuongezewa damu au kupewa vidonge ambavyo vingetuliza maumivu kwa muda,” anasema


Ilimchukua siku mbili kufika kwao Musoma na huko alianza kupatiwa matibabu, mpaka ilipofika Januari 11 alipoamka akiwa amepoteza uwezo wa kuona.

 

“Baada ya vipimo katika Hospitali za Muhimbili na CCBRT, daktari alishauri nipelekwe nje ya nchi kufanyiwa matibabu kwani hapa uwezo wao ulikuwa umefikia mwisho. Wazazi wangu walifanya mpango nikapelekwa Marekani, baada ya kufanyiwa operesheni nilianza kuona kwa mbali,” anasema na kuongeza:

 

“Nilipoteza uwezo wa kuona kwa zaidi ya mwezi mmoja, hivyo kuziona tena sura za familia yangu na ndugu zangu wengine, ilikuwa furaha ingawa siyo uono mzuri kama ule wa zamani.”

 

Margareth anasema kuwa anaamini kupoteza uwezo wa kuona siyo mwisho wa maisha, kwani ungekuwa ndiyo ukweli wenyewe, asingeweza kusoma Shahada ya Sheria na kuandika kitabu kwani vyote amevifanya.

 

“Kupoteza uwezo wa kufanya jambo lolote inaweza kuwa mwanzo mpya katika maisha yako. Nimemaliza shahada yangu ya sheria nchini Uingereza, nimeandika kitabu na kuanzisha Shirika lisilo la kiserikali la kusaidia wenye uono hafifu na wasioona liitwalo; Hope For The Blind ,” anasema na kuongeza:

 

Soma zaidi hapa: mwananchi.co.tz

Views: 316

Add a Comment

You need to be a member of Tulonge to add comments!

Join Tulonge

Comment by KUNAMBI Jr on January 14, 2014 at 12:22

atakua karogwa huyu si bure

Comment by Dixon Kaishozi on January 13, 2014 at 10:07

Nifunzo kubwa.. Pole yake na hongera yake kwani kwa haraka haraka inaonyesha ametoka kwenye "familia gani".  Mpaka kufikia kutibiwa MAREKANI. Hata harakati zake za masomo toka ameanza kuumwa umeona laikuwa nje ya nchi. Haya sasa kwa wenzangu na mimi.. nadhani safari yake ingeishia Musoma na ndiyo ungekua mwisho wa ndoto zake!!

Comment by Tulonge on January 12, 2014 at 7:45

Hili ni funzo tosha kwa baadhi ya watu. Kweli hujafa hujaumbika. Haya mambo ya kujidai/kuringa na kuwadharau wengine kwa jinsi wanavyoonekana kwa nje hayafai. Huwezi fahamu ni muda gani huo munekano wako mzuri unaweza badilika.

© 2020   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*