Tulonge

Kama hujui, wanaume ni wambea zaidi ya wanawake, tofauti ni kwamba wao hawasutani hadharani!

 

Katika jamii yoyote mtu mwenye tabia ya umbea huchukiwa, hutengwa na hata wakati mwingine hupigwa kwa kuonekana kuwa ni chanzo cha migogoro na huku viongozi wa dini wakimwona mtu wa aina hiyo kuwa ni mtenda dhambi.

 

Watu wanaopenda tabia ya umbea huenda wakawa wamepata mtetezi. Ripoti iliyotolewa hivi karibuni kuhusu tabia ya watu kupenda kutumia muda mwingi kusema mambo ya watu wengine, inasema tabia ya umbea ina manufaa kiafya.

 

Ripoti hiyo iliyotolewa na watafiti kutoka chuo kikuu cha Rhode Island cha Marekani, inasema kuwa watu wanaonufaika zaidi za tabia hiyo ni wale wanaopenda kuongea mambo mabaya wa watu wengine kuliko wenzao wanaopenda kuzungumza kuhusu mambo mazuri.

 

Wataalamu hao wamebaini kuwa iwapo mtu atatumia dakika 20 kuzungumzia mambo mabaya ya watu wengine, anaweza kuimarisha afya yake kwa kupunguza msongo wa mawazo, woga na mashaka kwa asilimia 96 kwa muda wa masaa manne mfululizo.

 

Hata hivyo, wamebainisha kuwa mtu akitumia muda huo huo kuzungumza mambo mazuri ya watu wengine, atapunguza msongo wa mawazo kwa asilimia 72 ikimaanisha kuwa watu wenye kuzungumza mambo mabaya ndio wenye kunufaika zaidi.

 

Watafiti hao, wakifafanua hali hiyo wameelezwa kuwa mtu anapoongea habari nzuri zinazowahusu watu wengine huuchochea ubongo kutaka kujiunganisha na mtu anayezungumzwa, wakati yule anayezungumza habari mbaya huwa kinyume chake.

 

Mtu anayezungumza habari mbaya anatabia ya kutokuhifadhi alichokisema, bali huendelea na mambo yake kama kawaida, wakati anayezungumza habari nzuri hukaa nazo moyoni kwa kipindi cha muda fulani.

 

Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Lusajo Kajula anasema binadamu wote huongea kuhusu watu wengine, lakini umbea ni zaidi ya maongezi.

 

Lusajo anasema asili ya mwanadamu ni kuzungumza japokuwa wakati mwingine hujikuta akiishia kutoa mifano halisi ya maisha ya watu wengine na hivyo kuingia katika mgogoro wakati mtu aliyesemwa anaposikia.

 

“Umbea ni kawaida na hauzuiliki, tatizo ni yaliyomo ndani ya umbea ambayo mara nyingi hutegemea na mawazo mtu aliyonayo. Kama ana mawazo hasi, ataongea mambo mabaya,” anasema Kajula.

 

Hata hivyo, Kajula anapingana na dhana iliyopo miongoni mwa watu kuwa mwanamke ndiyo anayependa zaidi tabia ya kuzungumza mambo ya watu wengine kuliko mwanaume.

 

“Kuna tafiti nyingi zinazoonyesha kuwa wanaume ni wambea zaidi kuliko wanawake, ila wao hawasutani na pia hawawezi kujieleza vizuri kama wanawake,” anasema Kajula na kuongeza kuwa kwa kawaida tabia ya kuongea mambo mazuri yanayowahusu watu wengine hukusudia kukuza heshima ya mtu anaezungumziwa.

Mwanasaikolojia na mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘Nguvu ya Umbea’, Maria Konnikova anasema hakuna mtu anaeweza kuukwepa umbea na kushauri kuwa mtu asihangaike kutaka kuwazuia wambea kusema wayatakayo.

Anasema wataalamu mbalimbali wa masuala ya saikolojia wamebaini kuwa umbea ni njia muhimu katika kuleta umoja na mshikamano katika jamii kwani kwa kufanya hivyo husaidia kueneza taarifa ambazo wanajamii wasingeweza kuzifahamu. “Pia imebainika kuwa umbea ni zana nzuri ya kuifundisha jamii mtu gani anafaa kuwa rafiki na yupi anastahili kuepukwa,” anasema Konnikova.

Mwanasaikolojia Homer Simpson wakati fulani aliwahi kusema: “Kama hatutakiwi kula nyama kwanini wanyama waliumbwa kwa nyama? Kama kila mtu anafahamu kuwa umbea ni mbaya kwa nini anasema? Jibu ni rahisi; katika ubongo wetu kuna sehemu inayopenda umbea.”

Anasema kila mtu ananufaika na mambo mazuri yanayosemwa juu yake anapoyasikia. “Wapi ungependa kufanya kazi, sehemu ambayo watu wanakusema vibaya au vizuri?”anahoji Simpson.

Mchungaji wa Kanisa la Free Pentekosti Tanzania (FPCT) Njia Panda ya Himo, Kilimanjaro, Elisante Ngailo, akizungumzia utafiti huo anasema watu wanaotumia muda mwingi kuzungumza mambo mabaya yanayowahusu watu wengine husema tu bila kufiria.

“Watu wa aina hii hawaumizi kichwa kufiri sana, wao husema mambo walioyasikia au kuyaona, kisha kuendelea na maisha yao,” anasema Ngailo.

Anaongeza: “Lakini hawa watafiti wanataka kutuambia kwamba sasa tuwaseme sana watu kusudi tupunguze msongo wa mawazo? Hili haliwezekani” anasema Ngailo.

Kwa maoni yake si sahihi kwa watu kuwasema watu wengine vibaya na kwamba tafiti kama hizi hazijengi jamii kwa kuwa tabia ya umbea inapingwa na makundi mbalimbali ya watu.

Chanzo: mwananchi.co.tz

Views: 958

Add a Comment

You need to be a member of Tulonge to add comments!

Join Tulonge

Comment by salum kitila on September 18, 2013 at 17:21

psycholocal eee,,

Comment by MGAO SIAMINI,P on June 30, 2013 at 17:14

jamani lakini umbea ni noma

Comment by Samwel Mnubi Masatu on June 29, 2013 at 9:22

mmmmm!

© 2023   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*