Tulonge

Chadema: Tutambana Spika mpaka kieleweke

MOTO wa kuwashtaki kwa wananchi Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai uliowashwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jijini Dar es Salaam Februari 10 mwaka huu, unatarajiwa kuendelea leo mjini Arusha ambapo chama hicho kitafanya mkutano mkubwa wa hadhara.

Mbali na mkutano huo, chama hicho kimesema Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah hana uwezo wa kutoa tamko kuhusu Bunge bila bunge lenyewe kuridhia, kusisitiza kuwa hata spika wa bunge naye hana uwezo wa kuunda Kamati za Bunge na kwamba wanachokifanya viongozi hao ni kudhoofisha Mamlaka ya mhimili huo wa Serikali.

Februari 8 mwaka huu Chama hicho kilitangaza vita kwa kwa viongozi hao wa bunge kwa madai kuwa wamezitupa hoja zilizowasilishwa bungeni na wabunge John Mnyika wa Chadema na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi.

Kutokana na hali hiyo kilitangaza kufanya maandamano nchi nzima ili kuwashitaki Makinda na Ndugai kwa kwa wananchi.

Mkutano huo ulifanyika Februari 10 katika viwanja vya Temeke mwisho jijini Dar es Salaam, huku viongozi wakuu wa chama hicho wakieleza yaliyojiri bungeni sambamba na kutaja namba za simu za Makinda hali iliyofanya baadhi ya wananchi kumtumia ujumbe wa matusi.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Willbroad Slaa alisema awali walitangaza kuwa mikutano hiyo itafanyika katika kanda 10, wanaanza na Kanda ya Kaskazini.

“Tunaanzia Arusha mjini na mkutano wetu utafanyika kesho, atakuwepo Mwenyekiti wa chama taifa, Freeman Mbowe pamoja na viongozi wengine wa chama” alisema Dk Slaa na kuongeza;

“Kila Kanda itakuwa na ratiba zake, lengo letu ni kufanya mikutano na kuwaeleza wananchi ukweli na tutakwenda hadi vijijini.”

Alisema mikutano hiyo kwa kila kanda inaweza kuchukua hadi mwezi mzima, huku akisisitiza kuwa kauli zinazotolewa na Makinda na Ndugai ni udikteta na kutaka kuiridisha Tanzania miaka 50 iliyopita.

Dk Slaa aliponda kitendo cha Makinda kuvunja baadhi ya Kamati za Bunge pamoja na Kashilillah kusema kwamba ofisi yake itazuia kuonyesha moja kwa moja vipindi vya Bunge, kabla ya juzi kuifuta kauli hiyo kwa maelezo kuwa sasa Bunge litaanzisha Televisheni yake na vituo vingine vitakuwa vikichukua matangazo ya bunge kupitia Televisheni hiyo.

“Nachokifanya Kashilillah ni kinyume na Katiba Ibara ya 18, Katibu wa Bunge hana uwezo wa kutoa tamko la kuzuia jambo fulani bila Bunge zima kuridhia mabadiliko hayo” alisema Dk Slaa na kuongeza;

“Hata Makinda naye hana mamlaka ya kuunda Kamati za Bunge, kifupi ni kwamba wanachokifanya ni kinyume na kanuni ya bunge ya 151(1) na 152(2).”

Alisema kuwa wakati akiwa mbunge, alikuwa mmoja wa watu walioshiriki kuzifanyia marekebisho baadhi ya kanuni lakini hivi sasa anashangazwa na jinsi Spika Makinda na wenzake wanavyozivunja waziwazi.

Alisema kuwa hata kama kutakuwa na Televisheni ya Bunge, bado watu watakuwa na mashaka kwa kuwa hawatajua nani ambaye atakuwa akisimamia urushwaji wa matangazo hayo.

“Huyo atakayekuwa akisimamia urushwaji wa matangazo hayo kwa upande wa Bunge ni nani, nani anayejua kuwa anaitikadi za chama gani au atapendelea mambo gani” alihoji Dk Slaa.

Alisisitiza, “Wanachokifanya ni ulevi wa madaraka na wanafanya maamuzi pengine kutokana na mawazo ya watu wengine.”

Hoja zilivyozimwa
Katika kikao cha bunge kilichomalizika hivi karibuni, Mnyika aliwasilisha Hoja Binafsi akilitaka Bunge liazimie kuitaka Serikali ichukue hatua za haraka kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo, hoja hiyo ilizimwa na Ndugai, ambaye baadaye aliruhusu kujadiliwa kwa hoja ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, hatua ambayo iliwafanya wabunge wote wa upinzani kusimama kwa pamoja na kuanza kupiga kelele za kupinga hatua hiyo ya Ndugai wakidai kwamba Naibu Spika huyo amevunja kanuni alizopaswa kuzisimamia.

Kitendo hicho pia kilisababisha kikao kuahirishwa kabla ya muda uliopangwa, huku hoja ya Profesa Maghembe ya kupendekeza kuondolewa bungeni kwa hoja ya Mnyika ikiungwa mkono na wabunge wa CCM.

Sambamba na tukio hilo Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia aliwasilisha hoja binafsi akidai serikali haina Mitalaa ya Elimu na kutaka Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza udhaifu huo.
Hata hivyo, hoja hiyo ilitupiliwa mbali, badala yake Ndugai aliunda kamati kuichunguza mitalaa hiyo kuangalia uhalali wake, kabla ya kuthibitishwa na Bunge.

Licha ya kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kuwasilisha bungeni mitalaa hiyo juzi, ambapo Mbatia alisema hakubaliani na mitalaa hiyo kwa maelezo kuwa kilichowasilishwa siyo kilichoahidiwa awali na Dk Kawambwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz

Views: 243

Add a Comment

You need to be a member of Tulonge to add comments!

Join Tulonge

Comment by Dixon Kaishozi on February 19, 2013 at 11:43

Kitaeleweka tu siku moja!!!

© 2021   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*