Tulonge

Kapuya arejea nchini bila kutiwa mbaroni

HATIMA ya Mbunge wa Urambo Magharibi Juma Kapuya (CCM), anayetuhumiwa kutishia kumuua binti anayedaiwa kumbaka, amerejea nchini jana akitokea nchini Sweden, huku Jeshi la Polisi likikwama kumtia mbaroni kama lilivyokuwa likitamba.
 
Wakati mbunge huyo akiwasili nchini na kupokewa na kusindikizwa na wapambe wake, Bunge limeridhia kukamatwa kwake kwani tuhuma zinazomkabili ni za jinai na zinamhusu yeye binafsi.
 
Mbunge huyo ambaye amepata kuwa waziri, amerejea nchini jana majira ya saa tano asubuhi kwa ndege ya Shirika la Qatar na kutua katika uwanja huo wa ndege na kuondoka kupitia mlango wa watu maarufu (VIP).
 
Habari zinasema mbunge huyo alipoondoka katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere alikwenda moja kwa moja kwenye moja ya hoteli za jijini Dar es Salaam na kuacha mizigo yake, kisha kuondoka na gari namba T 104 AEZ Toyota, huku wapambe wake wakiwa katika gari namba T 170 BGY aina ya Benz.
 
Wakati Kapuya akitua katika uwanja huo wa ndege, polisi ambao kwa takriban wiki moja sasa wamekuwa wakitamba kutaka kumtia mbaroni mara baada ya kutua, baadhi yao walionekana wakisalimiana naye kama vile hawakuwa wanamuwinda.
 
Tangu Profesa Kapuya alipoondoka nchini huku akizongwa na kashfa ya kutishia kumuua binti anayedaiwa kumbaka, polisi wamekuwa wakitamba kutaka kumtia mbaroni na kuahidi kuwa mara baada ya kurejea nchini mbunge huyo angekuwa chini ya ulinzi.
 
Tanzania Daima juzi liliripoti mkakati wa polisi kutaka kumtia mbaroni mbunge huyo mara atakapotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
 
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilisema kuwa kumekuwa na shinikizo kutoka ndani na nje ya jeshi hilo kutaka waziri huyo wa zamani ahojiwe kuhusiana na tuhuma zinazomkabili za kutishia kumuua binti anayedaiwa kumbaka.
 
Hatua ya polisi kutaka kumnasa Kapuya akiwa uwanja wa ndege inadaiwa kuchangiwa na taarifa ya  wiki iliyopita kwamba baadhi ya vigogo wa jeshi hilo walishiriki kufanikisha safari ya mbunge huyo nje ya nchi huku wakijua fika anatakiwa na polisi.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alipoulizwa kuhusu ujio wa Kapuya na kisha kuendelea kuachiwa huru, alisema yuko nje ya Jiji la Dar es Salaam na hakuwa na taarifa za kurejea kwake.
 
Hata hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Yusuph Mrefu, alipoulizwa kuhusu sakata la Kapuya, alisema hakuwa na taarifa ya kile kinachoendelea, kwa kuwa ndiyo kwanza amekabidhiwa ofisi.
 
“Mimi niambie jambo jipya, hapa ofisini ndiyo leo nimeingia kukaimu, sasa hayo mambo nitayajulia wapi, ni vema ungeniambia jambo jipya tuweze kutatua,” alisema Mrefu.
 
Kwa upande wake, Bunge limesema kuwa sakata la Profesa Kapuya lilifikishwa bungeni na kubaini kuwa ni la jinai, hivyo linapaswa kwenda kwenye mkondo wa kisheria.
 
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, alithibitisha kulifahamu suala hili, kwani binti aliyedai kubakwa na kutishiwa kuuawa na mbunge huyo alikwenda bungeni wakati Bunge la 13 lilipokuwa likiendelea mjini Dodoma.
 
“Suala la binti huyo lilifikishwa ofisini kwangu kupitia kwa msaidizi wangu ambaye  alisikiliza hoja na rai yake na kushauriwa kuwa hilo ni suala la jinai na linapaswa liende katika mkondo wa kisheria, hata hivyo binti huyo alitambulishwa kwa Spika kama kiongozi wa wabunge na kuelekeza kuwa tumshauri alifikishe katika mamlaka husika,” alisema Kashilila.
 
Tayari binti anayedaiwa kubakwa na kutishiwa kuuawa ameshafungua jalada namba OB/RB/21124/13 katika Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam na Jeshi la Polisi likaahidi kumkamata Kapuya popote alipo ili kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
 
Tayari makachero wa polisi wameanza kufuatilia namba ya simu inayodaiwa kutumika kumtisha binti huyo na wakati mwingine kutumika kurusha pesa kwa njia ya mtandao, zinazodaiwa kutoka kwa Profesa Kapuya kwenda kwa binti huyo.

Chanzo: Tanzania Daima

Views: 509

Add a Comment

You need to be a member of Tulonge to add comments!

Join Tulonge

Comment by habiba mustafa mlawa on December 2, 2013 at 9:26
huna jipya

© 2021   Created by Tulonge.   Powered by

Badges  |  Report an Issue  |  Terms of Service

/* \uascript type="text/javascript">\udinsert below header image\udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud \uascript type="text/javascript">\ud insert below header image \udif (typeof(x$) != 'undefined') {\ud var postHeaderImageAd = '\uadiv id="postHeaderImageAd ">\ua\ua/div>';\ud x$("#xg_masthead").after(postHeaderImageAd);\ud}\ud /*